
Dar es Salaam. Mlinzi Klabu ya The Voice Tz Limited, iliyopo Tabata Kinyerezi, jijini Dar es Salaam, Masoud Hassan, ameieleza Mahakama jinsi mshtakiwa Tumaini Moshi, alivyoficha vinywaji katika fulana yake ya bluu aliyoivaa, walipovamia katika klabu hiyo na kufanya vurugu akiwa na wenzake, Oktoba 29, 2025
Hassan ametoa ushahidi wake leo Jumatano, Februari 25, 2026 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikizwaji.
Mosha (33) na mwenzake Gasper Mmari (24), ambao wote ni wakazi wa Kinyerezi wilaya ya Ilala, wanakabiliwa na shtaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha na kujipatia vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh1.5 bilioni mali ya klabu hiyo.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali, Godfrey Odipoy, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo shahidi huyo alidai, Oktoba 29, 2025 akiwa kazini na wafanyakazi wengine muda wa saa 9 kwenda 10 jioni, ghafla waliona kundi la watu wakitokea upande wa Segerea wakielekea katika klabu hiyo.
Alidai, watu hao walishika mawe, mapanga, visu, madumu ya mafuta ya petroli, vipande vya nondo, matairi ya pikipiki, gari na walipofika eneo la upande wa kushoto, walianza kushambulia jengo.
“Wale watu waliturushia mawe, vipande vya nondo na matairi ya pikipiki ambayo yalikuwa yamechomwa moto ili tuuachie mlango waingie wao, lakini sisi tuliendelea kuwazuia.”
“Walisukuma geti wakitaka tuachie waingie ndani, nasi tulizuia, hata hivyo walionekana kutuzidi nguvu, nilipoona hivyo nilienda ofisi ya Mkurugenzi Benedict Kataluga, kumpa taarifa ambapo alipiga simu polisi Stakishari kuomba msaada” amedai Hassan.
Ameendelea kudai, watu hao wakiwa eneo hilo walifunga barabara kwa mawe na matairi ambapo polisi walipofika waliwatawanya kwa mabomu ya machozi ,wakaondoka.
Hassan amedai, hali ilipokuwa shari, polisi waliondoka na wao kuendelea na majukumu yao.
Amedai, ilipofika saa 12 jioni, kundi lingine la watu wakitokea Kinyerezi na Tabata lilifika tena wakiwa wamebeba mawe, marungu, madumu ya petroli na kushambulia jengo la baa hiyo kwa kasi wakipiga kelele, kurusha mawe na vipande vya gurudumu zilizo na moto.
Ameendelea kudai kuwa hawakuweza kuwazuia watu hao kwa sababu walikuwa wengi, hivyo walirudi nyuma ya jengo na kushuhudia uharibifu wa mali walioufanya ikiwa ni pamoja na kuvunja luninga, vinywaji, muziki, na vinginevyo.
Amedai, alitoka nje ya jengo ambapo alimuona mdada (Tumaini), amebebelea vitu alivyoweka katika fulana ya bluu aliyoivaa akiongozana na kijana mwenzake, na kisha akaongezeka mwingine na wote walipanda pikipiki na kutoweka.
“Nilipoona hivyo nami nilipanda pikipiki yangu nikiwa na wafanyakazi wenzangu wawili kuwafuatilia wale watu tujue walichobeba, vijana hao walienda umbali wa mita 50 hadi 60, walishuka katika pikipiki, tulipowafikia tuliwazunguka , kijana mmoja kati ya wale alijaribu kupigana nasi na alifanikiwa kutoroka,” amedai shahidi huyo.
Amedai, kijana wa pili aliilaza pikipiki chini na kuwaamuru wakae chini, alimpigia simu Kataluga ambaye alifika eneo hilo akiwa na askari.
Amedai vijana hao walikamatwa na wote walirudi katika klabu ya The voice ambapo walipekuliwa.
“Katika upekuzi huo, nilishuhudia yule dada aliyevaa fulana ya bluu akiwa anatolewa chupa nne za pombe kali aina ya Absolute Vodka na chupa moja ya bia aina ya safari, na simu huku yule kijana wa kiume alichukuliwa pikipiki aliyokuwa nayo aina ya Tvs nyeusi,” amedai shahidi huyo.
Akiendelea kutoa ushahidi wake, amedai pia askari walienda upande kuangalia katika kamera za CCTV na baada ya hapo wote walienda Kituo cha Polisi Stakishari kuandika maelezo.
Shahidi huyo aliendelea kudai, Novemba 7, 2025 alipeleka pikipiki mbili aina ya boxer kituo cha Polisi Stakishari, zilizokuwa zimetelekezwa katika maegesho ya baa hiyo.
“Zile pikipiki nilijua za wateja, lakini tulishauriana na bosi wangu na kuzipeleka Kituo cha Polisi Stakishari, zilikabidhiwa kwa afande Njau baada ya kuonekana hazina mwenyewe na kisha, niliandika maelezo ya ziada,” amedai
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi huu, hakimu Swallo ameahirisha kesi hadi Machi 3, 2026 itakapoendelea na ushahidi.