
Arusha. Mkuu wa Wilaya ya Arusha (DC), Joseph Mkude amesema Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wilaya hiyo, Dominic Mollel huku Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Morris Makoi akitoa ushirikiano wa kumtafuta dalali anayedaiwa kuchukua mali za aliyekuwa mfanyabiashara katika moja ya maduka ya stendi ndogo Arusha, Josephine Shirima.
Mwananchi imemtafuta mbunge huyo bila mafanikio kufuatia simu yake kuita bila kupokewa.
Jana Jumanne Februari 24,2026, mbele ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, Josephine alidai mbunge huyo na Mollel walihusika kushiriki kumdhulumu mali zake zilizokuwa dukani.
Dk Mwigulu alimwagiza DC Mkude kusimamia na kuhakikisha wahusika waliochukua mali hizo za Josephine wanazirudisha kisha ashughulikie masuala mengine yaliyokuwa yamesalia.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Februari 25, 2026, DC Mkude amesema wamewasiliana na Mbunge huyo ambaye yuko nje ya Mkoa wa Arusha na kuwapa ushirikiano mkubwa wa kumtafuta dalali wa Mahakama aliyetumika kwenda kuchukua mali hizo za mfanyabiashara huyo dukani kwake.
“Bado mali hazijarudishwa lakini tumewasiliana na Mbunge anakaa nje ya mkoa huu lakini ametupa ushirikiano mkubwa wa kumtafuta dalali wa Mahakama ambaye alitumika kwenda kuchukua mali hizo.”
“Dalali sasa hivi yuko njiani anatokea Moshi ataingia mchana huu akiingia atakwenda kuonyesha mali ambazo zinasemekana ziko stoo yule mama Josephine azitambue kama ni hizo na vipo katika hali gani,” amesema.
Mkude amesema baada ya hatua hiyo kesi ya msingi itaendelea dhidi yao kwani walichukua mali hizo bila kufuata taratibu za kisheria.
“Mollel anashikiliwa mpaka zipatikane hizo mali na sisi tumetoa muda mpaka mchana huu ziwe zimepatikana atakabidhiwa mbele ya watu na viongozi wa Serikali ili ahakiki kama ndiyo hivyo.”
Ilivyokuwa
Jana Jumanne Februari 24, 2026 akisikiliza kero za wananchi wa Jiji la Arusha katika eneo la Kilombero, Dk Mwigulu alitoa maagizo hayo baada ya Josephine kudai mali zake zilichukuliwa na mbunge huyo pamoja na Mollel.
Akiwasilisha changamoto hiyo, Josephine alidai kupangishiwa chumba na mbunge katika eneo hilo ambaye kwa kushirikiana na Mollel walivunja duka lake usiku wa manane na kuchukua mali zake.
“Nilikuwa na duka katika eneo la stendi ndogo ya Arusha mgogoro wa muda mrefu ambapo waliopewa maeneo hayo walijenga maduka kwa mkataba wa miaka 10, baada ya mkataba kuisha waliyarejesha halmashauri na kuanza kulipa kodi ambapo walikuwa wakitutoza kati ya laki tano hadi milioni moja na nusu.”
“Waliojenga wengine waliuza wakahamia Kariakoo, walionunua tukawa tunaweka kodi Sh500,000 hadi Sh1.5 milioni ila hawakuwa wanaipeleka halmashauri, kiukweli wametusumbua, wamefanya watu wengi kufilisika,” alidai.
Josephine alidai suala hilo linafahamika na uongozi kuanzia ngazi ya mkoa ila limeshindikana na kuomba asaidiwe arejeshewe mali zake zote kwani hawawezi kutokana na nguvu waliyonayo.
Kabla ya uamuzi huo, Dk Mwigulu alimhoji DC Mkude iwapo anafahamu suala hilo, ambaye alijibu kuwa anamfahamu mfanyabiashara huyo na aliwahi kufika ofisini kwake akilalamikia kudhulumiwa mali na watu wawili akiwemo kiongozi huyo pamoja na Mollel.
“Nilimwelekeza OCD afungue kesi ili suala lipelekwe mahakamani,” amesema Mkude huku akisisitiza hakuna ruhusa iliyokuwa imetolewa na mamlaka yoyote juu ya kuchukuliwa mali hizo bali wahusika walijichukulia mamlaka mkononi,” amesema.
Waziri Mkuu alihoji sababu za kufunguliwa kesi ilihali mali zilichukuliwa bila ruhusa na kusisitiza wahusika wanapaswa kuzirejesha haraka na kumwagiza Mkude kushughulikia masuala mengine yanayohusiana na mgogoro huo baada ya mali hizo kurudishwa.
“Watafute mpaka jioni mali ziwe zimesharudishwa na nimeelekeza kote asiwepo mtu anayechukua mali ama kitendea kazi cha mtu, watafute huyu Mollel yuko wapi? DC elekeza aliyeshikilia hizo mali arudishe leoleo na baada ya mali kurudishwa shughulikia haya mengine yaliyokuwa yamesalia, naombeni zile nyaraka nizipate mwenyewe,” amesema.
Mollel aliyekuwa kwenye mkutano huo, alipoulizwa alidai Josephine alikuwa mpangaji wa huyo kiongozi ila hakuwa analipa kodi na kuwa kwa kipindi hicho walimwomba Mkuu wa wilaya, kuwa watu 10 wasiokuwa wanalipa kodi akiwemo huyo mama wafuatiliwe.
Alidai suala hilo lilifikiwa na walitakiwa wafuate taratibu na sheria ambapo OCD alitoa askari na magari mawili pamoja na dalali wa Mahakama na vitu hivyo vilichukuliwa na dalali huyo, na kudai Josephine alitakiwa kwenda kuvichukua ila ameshindwa kwa sababu hana fedha.
Hata hivyo, alipopewa nafasi tena, Josephine alipinga maelezo hayo akidai wakati mali zake zinachukuliwa hakukuwa na askari polisi eneo la tukio isipokuwa baada ya kuvunjwa askari walifika eneo hilo na Mollel akakamatwa, ambapo alipoachiwa baadaye ndipo walienda kuchukua mali zake.
“Mkuu wa wilaya alisema huu ni wizi kama wizi mwingine, Polisi nilifika nikapigwa danadana ikaja ikafunguliwa kesi ambayo sijui ilikuja kuishaje, nakwambia hawa watu wana nguvu ingia youtube angalia speech anazotoa huyu baba (Mollel) anatishia mpaka Serikali ni watu siwawezi,” amedai.
“Tumia vyombo, fanya uchunguzi sikudanganyi na wameumiza watu wengi, mikataba nimekupa na kodi mimi ni mwananchi wa Arusha nimezaliwa na kuishi najua ninachokueleza,” alihitimisha.