Naanza uchambuzi huu kwa kuweka wazi msimamo wangu: ninaafiki rai ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, kwamba tusizidi kuyachimbua kwa kina matukio ya Oktoba 29, 2026 ili kuepusha kuendeleza majeraha ya kitaifa.

Hata hivyo, kwa kuwa tupo katika kipindi ambacho dini kuu mbili nchini, Ukristo na Uislamu zinaadhimisha mfungo na toba, nimeona kuna umuhimu wa kulitazama tukio hilo katika mwanga wa tafakari ya kiroho na uwajibikaji wa dhamira.

Kwa Wakristo, hiki ni kipindi cha Kwaresma; siku 40 za kufunga, kutafakari na kutubu. Kwa Waislamu, ni mwezi mtukufu wa Ramadhani; siku 29 au 30 za saumu, dua na mageuzi ya nafsi.

Mara chache vipindi hivi hukutana kwa wakati mmoja. Kukutana kwake mwaka huu kunaweza kutazamwa kama mwaliko wa pekee kwa taifa kufanya tathmini ya kina, si tu ya matendo, bali pia ya mioyo yetu.

Swali langu ni hili: Je, tutumie kipindi hiki kufanya toba ya kweli, kila mmoja akijichunguza, akakiri makosa yake, akajuta na kuomba msamaha kwa Mungu ili taifa litakasike?

Au tusubiri matokeo ya Tume ya Uchunguzi ili itamke iwapo kulifanyika makosa, ndipo wahusika wajitokeze kuomba radhi na kuanzisha mchakato wa maridhiano?

Kwa mujibu wa mafundisho ya dini hizi mbili, wanadamu wote ni watoto wa baba mmoja. Simulizi za mwanzo zinamtaja Adamu na Hawa kama wazazi wa kwanza wa ubinadamu.

Hata neno mwanadamu hubeba dhana ya mwana wa Adamu. Ujumbe wake ni mmoja: asili yetu ni moja na hivyo maumivu ya mmoja yanapaswa kuwa maumivu ya wote. Tunapoumizana, tunajiumiza; tunapoponya, tunajiponya.

Vivyo hivyo, simulizi ya Nabii Ibrahim inaheshimiwa katika imani zote mbili. Alibarikiwa watoto wawili, Ismaili na Isaka ambao kwa mapokeo ya kidini wanahusishwa na chimbuko la Waislamu na Wakristo.

Tofauti zipo katika baadhi ya tafsiri, ikiwamo kuhusu mwana aliyekusudiwa kutolewa sadaka. Waislamu huamini alikuwa Ismaili, jambo linalokumbukwa katika Sikukuu ya Eid al-Adha; Wakristo huamini alikuwa Isaka na Kwaresma huhitimishwa kwa kumbukumbu ya mateso na kifo cha Yesu Kristo msalabani kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu. Pamoja na tofauti hizi, funzo kuu ni utiifu, imani na utayari wa kujitoa kwa ajili ya yaliyo mema.

Katika ukoo huo, ndipo alipoibuka Nabii Musa, aliyewakomboa Wanaisraeli kutoka utumwani Misri na kupokea Amri Kumi.

Sheria hizo za maadili zilizomo katika Taurati na kuheshimiwa pia katika Ukristo, zinabaki kuwa dira ya mwenendo mwema.

Hivyo, tunapozungumzia toba hatuzungumzii jambo la pembeni; tunarejea kwenye msingi wa imani zetu unaotutaka kutenda haki, kupenda rehema na kuenenda kwa unyenyekevu mbele ya Mungu.

Baada ya tukio la Oktoba 29, taifa limebeba huzuni sintofahamu na maumivu, hasa kutokana na taarifa za umwagikaji wa damu. Hali kama hii inahitaji zaidi ya uchunguzi wa kisheria; inahitaji pia uchunguzi wa dhamira.

Sheria inaweza kubaini ukweli wa matendo na kubainisha uwajibikaji wa kiserikali, lakini toba ya kweli huanzia moyoni mwa mhusika. Dhamira haingoji ripoti; huzungumza papo hapo.

Ndiyo maana nasisitiza, toba ninayoizungumzia hapa si ya kusubiri tamko la chombo chochote. Ni toba ya mtu binafsi mbele ya Mungu wake. Ikiwa umetenda kosa, unalijua.

Nafsi yako inakushuhudia. Juta, kiri, omba msamaha na uwe tayari kuwajibika. Kuwajibika si udhaifu; ni ujasiri wa kimaadili. Pale ambapo kuna madhara, fidia na maridhiano ya kweli ni sehemu ya safari ya uponyaji.

Kusubiri ripoti ya Tume ya Uchunguzi kuna nafasi yake katika muktadha wa kisheria na kiutawala. Lakini utakaso wa taifa haucheleweshwi na ratiba za taasisi.

Huanzia kwenye mioyo ya watu wake. Ikiwa kila mmoja atatumia kipindi hiki kuondoa chuki, kurekebisha alikokosea na kuomba msamaha kwa dhati, tutakuwa tumeanza kujenga taifa linalosimama juu ya haki na upendo.

Kwa Wakristo, nawatakia Kwaresma yenye tafakari na mageuzi. Kwa Waislamu, Ramadhani yenye rehema na baraka. Tuitumie fursa hii kufanya toba ya kweli kwa nafsi zetu na kwa ajili ya taifa.

Mungu ibariki Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *