KIUNGO wa Tanzania Prisons, Abdallah Masoud ‘Cabaye’ ambaye kwa sasa yupo nje ya uwanja akiuguza jeraha la goti ameweka wazi kuwa bado ana matumaini makubwa ya kurejea mapema kuisaidia timu hiyo kupambana na hatari ya kushuka daraja.

Cabaye alipata jeraha hilo Novemba 26, 2025 wakati Tanzania Prisons ilipokubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate katika mechi ya Ligi Kuu Bara. Tangu siku hiyo, amekuwa nje ya uwanja akiendelea na matibabu huku akifuatilia kile kinachoendelea kwa timu hiyo.

“Niligongana na Mokono (Elie), ilikuwa kipindi cha kwanza cha mchezo, mwanzo nilihisi kwamba labda ni maumivu ya kawaida lakini ikawa tofauti,” alisema na kuongeza;

“Nimekuwa nikiumizwa na matokeo ya timu lakini naamini tunaweza kukaa sawa na kujiondoa katika hatari ya kushuka daraja.”

Tangu kuumia kwa Cabaye, Prisons imecheza mechi nane za ligi, imeshinda moja dhidi ya Namungo kwa mabao 3-2.

Matokeo hayo yameifanya timu hiyo kuendelea kusuasua kwenye msimamo wa ligi, ikiwa nafasi ya 14 na pointi 12 kati ya timu 16.

Kiungo huyo mkabaji anatakiwa kukaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki sita hadi nane kwa mujibu wa ushauri wa madaktari.

Hata hivyo, ameeleza kuwa anafanya mazoezi mepesi na kufuata maelekezo yote ya kitabibu ili kurejea mapema kadiri itakavyowezekana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *