
Ruvuma. Jumla ya wapigakura 127,632 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi utakaofanyika kesho Februari 26, 2026 kwa ajili ya kumchagua mbunge wa Jimbo la Peramiho na diwani wa Kata ya Shiwinga.
Uchaguzi wa Peramiho unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jenista Mhagama (CCM) aliyefariki dunia Desemba 11, 2025.
Akizungumza leo Februari 25, 2026 mjini Songea, mkoani Ruvuma, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele, amesema maandalizi ya uchaguzi huo yamekamilika.
Amesema wapigakura 120,780 wamejiandikisha katika Jimbo la Peramiho na 6,852 katika Kata ya Shiwinga.
Amesema jumla ya vituo 373 vya kupigia kura vitatumika na 354 vipo katika Jimbo la Peramiho na 19 katika Kata ya Shiwinga, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.
Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, vyama vya siasa 15 vimesimamisha wagombea katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Peramiho, huku vyama vinane vikisimamisha wagombea katika uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Shiwinga.
Ametumia fursa hiyo kuvikumbusha vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo kuzingatia wajibu wao wa kuteua mawakala katika vituo vyote vya kupigia, kuhesabu na kujumlisha kura. Amesema wasimamizi wa uchaguzi katika jimbo na kata husika wamekamilisha taratibu zote zinazowezesha mawakala kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi kwa uwazi.
Aidha, amesema mawakala wanawajibika kulinda masilahi ya vyama na wagombea wao, hivyo wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi pamoja na maelekezo ya Tume wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Jaji Mwambegele amesema vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.
“Ifikapo saa 10:00 jioni kama bado kutakuwa na wapigakura waliopanga mstari, mlinzi wa kituo atasimama nyuma ya mpigakura wa mwisho na hatua ya upigaji kura itaendelea hadi waliokuwapo kwenye mstari watakapomaliza kupiga kura,” amesema.
Amesisitiza kuwa baada ya kupiga kura, mpigakura anatakiwa kuondoka katika eneo la kituo, na akiwa kituoni anatakiwa kufuata maelekezo atakayopewa na karani mwongozaji wa wapigakura.
Kwa upande wa utambulisho, amesema mpigakura aliyeandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na ambaye taarifa zake zipo katika daftari la kituo husika, lakini amepoteza au kuharibu kadi yake ya mpigakura, ataruhusiwa kupiga kura kwa kutumia kitambulisho chochote kati ya Kitambulisho cha Taifa (Nida), leseni ya udereva au hati ya kusafiria (pasipoti).