Dodoma. Serikali imesema ni ruksa kwa wanafunzi waliopewa ufadhili wa masomo ya sayansi nje ya nchi, kama watapata kazi huko baada ya kumaliza masomo ili mradi wapate kipato kinachoendana na ujuzi wao.

Mbali na ruhusa hiyo, Serikali pia imewaita wadau wa elimu, benki, migodi na taasisi kwenye nia ya kusaidia ufadhili wa masomo ya sayansi ili waweze kukaa pamoja na kujadiliana namna bora ya kumsaidia mtoto wa Kitanzania.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Februari 25, 2026 na Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda wakati akizungumzia ufadhili wa wanafunzi wa masomo ya sayansi ambao baadhi yao tayari wako katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Profesa Mkenda amesema Serikali haiwabani wanafunzi waliopatiwa ufadhili wa masomo kwamba lazima warudi na kuja kufanya kazi nchini, kwani inatambua kuwa hata wakifanya kazi huko bado watarudi na ujuzi zaidi isipokuwa wanapaswa kuwa na uzalendo.

“Kwa mfano mtu akipata kazi huko baada ya kumaliza masomo yake unawezaje kumzuia je, akirudi hapa nchini unakwenda kumpa kazi gani yenye mshahara sawa na kule, sisi tunachowaomba ni kuwa na uzalendo kwa nchi yao ili siku wakisema wanarudi ndiyo wanakuwa na ujuzi wa hali ya juu,” amesema Profesa Mkenda.

Waziri amesema ufadhili wa masomo ya sayansi kwa Serikali unaendelea na hivi karibuni watachukuliwa wanafunzi 50 watakaopelekwa nchini Ireland na wengine watapelekwa chuo cha Indian Istitute Of Technology tawi la Zanzibar.

Kuhusu namna ya kuwapata, amesema Serikali kwa sasa imebadili mfumo kwani inaangalia matokeo ya mitihani kwa wanaokwenda kuanza shahada ya kwanza na kuwatafuta yenyewe, huku ikiachia uwanja kwa wale wanaokwenda shahada ya pili ili vyuo viweke masharti ingawa Serikali itatupia jicho lake.

Wanafunzi hao wanapelekwa katika vyuo hivyo vya kimataifa ikiwa imepita muda mfupi tangu Serikali ilipowapeleka wanafunzi wengine wa masomo ya sayansi katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST).

Amesema katika dunia ya sasa nchi itakayobaki nyuma katika sayansi itakuwa na taabu mbeleni, hivyo Tanzania imeamua kuwekeza kwa ukamilifu katika eneo la sayansi ndiyo maana inachukua wanafunzi wenye ufaulu wa juu bila kujali wanatoka shule za Serikali au binafsi.

Kwa mujibu wa Mkenda, katika bajeti ya 2025/26 zilitengwa jumla ya Sh5 bilioni kwa ajili ya ufadhili huo ambao umeonyesha matunda huku wanafunzi kutoka sekondari zinazoitwa za kata wakiendelea kuchomoza zaidi.

Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Maulilo Kipanyula amesema Chuo hicho kinachukua wanafunzi kulingana na uwezo wao na hakuna namna wanavyoweza kupokea mtu asiyefikia viwango.

Profesa Kipanyula ametolea mfano wa wanafunzi 10 ambao wamepokelewa hivi karibu kwamba walifanyishwa mtihani kwanza na baada walitakiwa kila mmoja kuwa na andiko litakaloelezea nini matarajio ya Watanzania katika elimu watakayopewa, na ndipo wakapatikana waliotakiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) , Dk Amos Nungu amesema Tanzania imeendelea kupewa nafasi zaidi na vyuo vikuu duniani wakiomba kupatiwa wanafunzi kwani waliopelekwa nje ya nchi wamekuwa wakifanya vizuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *