Tanga. Mwaka 2007 wakati Kitongoji cha Chang’ombe, kilichopo Kijiji cha Mkata Magharibi, wilayani Handeni, Tanga kikiwa kinapambana kujenga misingi ya huduma za kijamii, ndoto ya kuwa na shule ya kisasa ilizaliwa.
Kwa msaada wa Shirika la World Vision, Shule ya Msingi Imani ikajengwa mita 300 kutoka barabara kuu inayounganisha mikoa ya Kaskazini na nchi jirani. Ilikuwa fahari ya kijiji na alama ya matumaini ya kizazi kipya.
Miaka ilivyopita, idadi ya wanafunzi iliongezeka hadi kufikia zaidi ya 1,000. Lakini majengo hayakuongezeka kwa kasi hiyo, nyufa zikaanza kuonekana ukutani, sakafu zikiwa za michanga na hatimaye madarasa matatu yakafungwa kwa amri ya mhandisi, baada ya kubainika ni hatarishi kwa usalama wa watoto.
Mbali ya changamoto hizo, kwa mujibu wa matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2025, shule hiyo imeongoza kati ya shule tatu za Serikali zilizopo katika Kijiji cha Mkata Magharibi.
Changamoto zilivyoanza
Kwa zaidi ya miezi minne tangu Septemba 24, 2025 wanafunzi wamelazimika kusoma kwa zamu, huku darasa la kwanza na la awali wakisomea nje, chini ya miti. Mvua ikinyesha masomo yalikatizwa.
Muonekano wa madarasa ya Shule ya Msingi Imani iliyopo Mkata Magharibi, Tanga.
Darasa la pili, tano na sita yalibadilishana vipindi kulingana na upatikanaji wa chumba.
Kutokana na hali hiyo, wazazi hawakukaa kimya walichanga Sh5, 000 kila mmoja kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili lakini waliishia kwenye darasa moja ambalo walikamilisha boma na Serikali ikapaua.
Akizungumza na Mwananchi Februari 23, 2026 Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chang’ombe ilipo shule hiyo, Said Machokoro amesema awali shule ilikuwa na madarasa sita, ofisi na nyumba ya walimu.
Hata hivyo, madarasa matatu yalisimamishwa kutumika baada ya kubainika kuwa ni hatarishi kwa usalama wa wanafunzi.
Kutokana na hali hiyo, wanafunzi walibaki wakitumia madarasa manne pekee, likiwamo moja lililokamilika kwa nguvu za wananchi, hivyo watoto kulazimika kusoma kwa zamu.
Amesema kuna wakati hulazimika kuingia kwenye darasa moja endapo mwalimu atakuwa na vipindi kwa madarasa yote, huku wengine wakikaa chini.
“Wakati wa mvua hali huwa mbaya zaidi, walimu wanatumia nguvu kubwa kupanga ratiba ili kila mtoto apate nafasi ya kujifunza. Watoto hujikuta wanaingia kwenye darasa moja, huku wengine wakikaa chini,” amesema.
Ameeleza shule hiyo iliyojengwa mwaka 2007 kwa msaada wa World Vision imekuwa na kasoro kadhaa, vilijengwa vyoo vya matundu 10 lakini vilibomolewa kutokana na uchakavu. Kutokana na msaada wa Shirika la Amref, kulijengwa vyoo vya matundu saba.
Mbali na madarasa, amesema nyumba ya mwalimu pia ni chakavu na haitumiki kwa sasa kutokana na hofu ya usalama, hali inayosababisha watumishi hao wakose makazi ya uhakika jirani na shule.
Amesema kutokana na hali hiyo wazazi na wadau wamekuwa wakijitolea michango kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ambayo ilifanikisha ujenzi wa darasa moja kati ya mawili waliyokubaliana kujenga.
Mzazi wa wanafunzi watatu katika shule hiyo, Saidi Kigua amesema kabla ya msaada wa Serikali, wazazi walikuwa wakichanga fedha kwa awamu ili kujenga na kukarabati madarasa.
“Tulichanga Sh5,000 kila mzazi, baadaye tukachanga tena kwa ajili ya matofali na saruji. Hadi sasa bado tunaendelea kuchanga kwa ajili ya matofali, kila mzazi akitoa takribani Sh1, 200,” amesema.
Kigua amesema mchango wa kwanza ulilenga kujenga madarasa mawili lakini walijenga moja, wakiendelea na michango kwa kupeleka tofali mbili.
“Nina watoto watatu hapa, wakati mwingine wanapaswa kusoma kwa zamu, wengine chekechea wanasomea nje na wanakaa chini kwa kukosekana madawati. Mvua ikinyesha ni shida kubwa,” amesema.
Licha ya juhudi hizo za wazazi, bado kuna tatizo la madawati kama linavyoelezwa na wanafunzi mmoja (jina linahifadhiwa) kuwa wamekuwa wakikaa chini, huku wakiingia darasani baada ya kuvua viatu.
“Tukiingia darasani tunavua viatu ili wanaokaa chini wasichafuke. Wengine walikuwa wanasomea nje lakini kwa sasa wote tunaingizwa darasani,” amesema.
Ziara yaleta neema
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkata Magharibi, Mussa Ngana aliibua hoja ya ubovu wa madarasa matatu ambayo hayatumiki kutokana na marufuku iliyotolewa na mhandisi.
Muonekano wa madawati ya Shule ya Msingi Imani iliyopo Mkata Magharibi, Tanga.
Ngana alisema shule hiyo kwa sasa inatumia madarasa manne pekee, huku zaidi ya wanafunzi 1,000 wakilazimika kubanana, hali inayohatarisha ubora wa elimu.
“Nimechoka kujibu hoja za wananchi kutokana na kikomo changu cha uongozi, hivyo ziara yako itakuwa msaada wa kutatuliwa kwa tatizo hilo,” alisema Ngana.
Mbali ya madarasa, pia nyumba ya mwalimu imeelezwa kuwa chakavu na isiyofaa kwa matumizi.
Sauti hiyo ilisikika Februari 13, 2026, wakati Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alipokuwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Tanga, alikoweka jiwe la msingi la kituo cha kupoza umeme Mkata.
Alipopokea taarifa ya uchakavu wa madarasa, hakusita kutoa maelekezo.
“Mwandikie kabisa katibu mkuu, mwisho wa mwezi hizo fedha ziwe zimefika na mkurugenzi anasikia na mkuu wa mkoa, fedha zitatoka wapi, wakate safari wakate chaichai kila mtu anywe chai nyumbani kwake, fedha hizo zije tutengeneze kizazi cha kesho hapa,” aliagiza Dk Mwigulu.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe alisema tayari amemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni Vijijini kupeleka Sh50 milioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili.
Alisema amemwelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kupeleka Sh50 milioni nyingine ili kuongeza madarasa mawili zaidi, hivyo kufikisha jumla ya madarasa manne yatakayojengwa.
Akizungumza na Mwananchi Februari 23, 2026 Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni, Glasness Mwano alisema wametenga Sh50 milioni kama ilivyoelekezwa na Waziri wa Tamisemi na pia wamepokea Sh50 milioni kutoka wizarani Februari 16, 2026.
Amesema fedha hizo zitajenga madarasa manne, mawili kwa fedha za halmashauri na mawili kwa fedha za Tamisemi pamoja na ununuzi wa madawati.
“Baada ya tamko la Waziri Mkuu tulichukua hatua, Februari 14, 2026 kwa kushirikiana na wananchi shughuli ilishaanza na Jumatatu ya Februari 16, mwaka huu, mkurugenzi alifika eneo husika na alisaidiana na wananchi,” amesema Mwano.
Tumaini jipya
Gazeti la Mwananchi limefika katika Shule ya Msingi Imani na kukuta ujenzi ukiendelea, likielezwa ulianza siku ya pili baada ya Waziri Mkuu kutoa agizo.
Mjumbe wa Kamati ya Ujenzi, Juma Kiondo amesema ujenzi ulianza mapema baada ya agizo kutolewa, hivyo ni tumaini jipya kwa wanafunzi na wazazi kwani walikuwa wanachangishana kwa muda mrefu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.
“Ujenzi huu utachukua muda mfupi kwa jinsi tulivyoelezwa lakini bado tutaendelea kwa darasa letu ambalo lilibaki kwa sababu wazazi walishaanza kuchanga matofali na utaratibu sisi tunajenga boma, Serikali inamalizia,” amesema Kiondo.
Mwenyekiti wa Kitongoji, Machokoro amesema kwa sasa wananchi wa Chang’ombe na Mkata Magharibi, wanaeleza matumaini kuwa ujenzi wa madarasa manne utamaliza adha ya wanafunzi kusoma kwa msongamano na kwa zamu.
Vilevile, utarejesha hadhi ya shule hiyo iliyo kando mwa barabara kuu inayounganisha mikoa na hata nchi jirani.
“Tunamshukuru Waziri Mkuu kwa kutukumbuka, hii italeta picha mpya ya shule yetu na kuinua morali ya walimu na wanafunzi,” amesema.
Machokoro amesema utekelezaji huo wa haraka unaonekana kuwa mfano wa namna uamuzi kutoka ngazi ya juu unavyoweza kubadilisha hali halisi ya wananchi kwa muda mfupi, hasa katika sekta ya elimu ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa.
Muonekano wa madarasa ya Shule ya Msingi Imani iliyopo Mkata Magharibi, Tanga.
Mbali ya hayo, Machokoro amesema kumekuwa na makubaliano ya maneno kati ya shule na mradi wa umeme uliotumia eneo la shule kwa muda, kwamba wajenge jengo la madarasa kufidia matumizi ya eneo hilo.
“Hali hii imesaidia maana wamejenga madarasa ambayo wameyafanya ni ofisi yao kwa sasa, baada ya mradi kukamilika watayakabidhi kwa shule ili yaweze kutumika,” amesema.