
Moshi. Madereva daladala eneo la Njia Panda, Himo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, waligoma kwa zaidi ya saa tano wakidai madereva bajaji kuwanyang’anya abiria katika vituo vyao vya kupakia na kushusha abiria barabara ya Marangu–Mwika.
Mgomo huo ulitokea Februari 25, 2026 na kusababisha usumbufu kwa wasafiri, huku daladala zikisitisha huduma zikishinikiza bajaji kuondoka katika eneo lao. Hali hiyo ililazimu Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, kuingilia kati.
DC Mnzava aliwaagiza madereva bajaji kurejea katika eneo lao la awali la Bavaria ili kuondoa mwingiliano huo, huku akiwataka madereva daladala kuendelea na kazi ili kuepusha adha kwa wananchi. Pia alisisitiza kuitishwa kikao cha pamoja cha wadau, wakiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) na Polisi wa Usalama Barabarani, kutafuta suluhu ya kudumu.
Kwa upande wa daladala, Katibu wa Umoja wa Madereva Moshi–Marangu, Venance Minja, amesema kumekuwa na sintofahamu kuhusu mipaka ya shughuli za kila upande, akidai bajaji kufanya kazi kama daladala jambo linalozua msuguano.
Naye mwakilishi wa madereva bajaji Himo, Peter Mjema, amesema wanakabiliwa na changamoto ya kukosa kituo rafiki cha kupaki, hali iliyowalazimu kusogea karibu na eneo la daladala, akisisitiza kuwa wako tayari kwa mazungumzo ili kupata mwafaka.