Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema imeridhishwa na mwenendo wa wafanyabiashara kuuza bidhaa kwa kuzingatia bei elekezi zilizowekwa na Serikali katika kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Februari 25, 2026 na Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Shariff Ali Shariff, alipofanya ziara ya kukagua masoko mbalimbali ikiwemo MwanaKwerekwe, Darajani, Mombasa na Jumbi.

Shariff amesema ziara hiyo imelenga kukagua upatikanaji wa bidhaa muhimu zinazohitajika zaidi katika mwezi wa Ramadhani pamoja na hali ya bei zake kwa wananchi wa Unguja.

“Nimeridhishwa kuona wafanyabiashara wengi wametii agizo la Serikali kwa kufuata bei elekezi walizopangiwa. Kwa mfano, kilo moja ya mchele wa pembe inauzwa kwa Sh1,800, sukari Sh2,400, unga wa ngano kilo moja Sh1,800 na lita moja ya mafuta Sh5,500. Wapo hata waliouza chini ya bei hizo, jambo tunalolipongeza,” amesema.

Aidha, amesema Serikali ilitoa agizo la kuwataka wafanyabiashara kuweka vibango vinavyoonesha bei za bidhaa zao ili kurahisisha uwazi kwa wanunuzi, na kwa kiasi kikubwa maelekezo hayo yamezingatiwa.

Kwa mujibu wa Kaimu Waziri huyo, hali ya upatikanaji wa chakula upande wa Unguja ni nzuri, ingawa changamoto iliyopo ni uwezo mdogo wa baadhi ya wananchi kumudu gharama za kujinunulia mahitaji yao.

Amesema hali hiyo si ya Zanzibar pekee, bali ni changamoto inayotambulika kimataifa kutokana na tofauti za kiuchumi miongoni mwa watu.

Amesema Serikali baada ya kulitambua hilo, imechukua hatua ya kupunguza ushuru kwa waingizaji wa bidhaa mbalimbali ili kupunguza makali ya bei na kuwezesha wananchi kumudu gharama za maisha katika kipindi hiki cha Ramadhani.

Hata hivyo, licha ya kuridhishwa na mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula vikuu, amesema bado kuna malalamiko kuhusu bei za kitoweo ikiwemo samaki, nyama na kuku.

Kwa sasa, kilo moja ya nyama inauzwa kwa Sh18,000, kuku mmoja kwa Sh10,000 huku bei ya samaki ikitegemea ukubwa wake. Serikali imeahidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo ili kupunguza malalamiko ya wananchi.

Shariff pia amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili kubadilisha mitazamo ya kizamani na kuwahamasisha kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika uendeshaji wa biashara zao.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani Halali wa Biashara Zanzibar (ZFCC), Alya Emanuel Juma, amesema ziara hiyo imelenga kufuatilia utekelezaji wa bei elekezi zilizowekwa kwa ajili ya mwezi wa Ramadhani.

Amesema tume hiyo inawataka wauzaji wote kubandika bei za bidhaa zao waziwazi ili kumuondolea usumbufu mnunuzi, na yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa mujibu wa Sheria Namba Tano ya mwaka 2018, wafanyabiashara wanatakiwa kubandika bei kwenye bidhaa zote ili mteja aweze kuiona bei moja kwa moja badala ya kutajiwa na muuzaji.

“Bei elekezi inapaswa kuwekwa kwa kila bidhaa kwa kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao huwatazama wateja na kupanga bei wanazotaka wao,” amesema Alya.

Naye mwananchi Issa Ussi Haji, amesema kwa sasa hali ya bei za bidhaa si ya kupanda kupita kiasi na wananchi wengi wanaweza kumudu kununua mahitaji ya futari.

Hata hivyo, amesema bei ya nyanya imepanda ambapo kilo moja inauzwa kati ya Sh1,500 na Sh2,000, karoti kilo moja Sh1,500 na vitunguu maji kati ya Sh2,000 na Sh2,500, huku bidhaa nyingine zikiendelea kuuzwa kwa bei ya kawaida.

Mfanyabiashara wa soko la Kwerekwe, Muslim Harith amesema biashara imeimarika na wateja wameongezeka kwa ajili ya maandalizi ya Ramadhani.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kuendelea kuzingatia bei elekezi za Serikali ili mwezi huo uwe wa ibada na faraja kwa waumini, badala ya kuwaongezea mzigo wa gharama za maisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *