Dar es Salaam. Wizara ya Afya imetoa tahadhari kwa wananchi kufuatia ongezeko la wagonjwa wa mafua makali na Uviko-19 nchini, huku ikiwasihi kuchukua hatua za kinga ili kudhibiti maambukizi.

Serikali pia imeonya kuhusu hatari ya Homa ya Dengue kufuatia mvua za masika zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini, hali inayochochea mazalia ya mbu aina ya Aedes.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano, Februari 25, 2026 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe.

Tahadhari hiyo inatolewa kukiwa na ongezeko la watu wanaopata mafua na magonjwa mengine yanayohusiana na njia ya hewa kama homa, kikohozi, na baridi hasa wakati huu wa mabadiliko ya msimu.

Magembe amesema takwimu za ufuatiliaji zinaonyesha kuwa kila mwaka kuanzia Novemba hadi Aprili kumekuwa na ongezeko la maambukizi ya mafua makali ya Influenza na Uviko-19, hali inayoshuhudiwa pia katika nchi nyingine duniani.

Ameeleza kuwa magonjwa hayo huenezwa kupitia majimaji yanayotoka kwenye njia ya hewa ya mgonjwa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza na pia kwa kugusa maeneo yaliyochafuliwa.

Amezitaja dalili zake ni pamoja na homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu.

“Wizara inazitaka jamii kufunika pua na mdomo wanapokohoa au kupiga chafya, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, kuvaa barakoa wanapokuwa na dalili au wakiwa kwenye maeneo yenye msongamano, pamoja na kuzingatia usafi binafsi na wa mazingira,” ameelekeza.

Aidha, wananchi wametakiwa kuwahi vituo vya afya kupata matibabu na kuepuka kutumia antibiotiki bila ushauri wa wataalamu.

Dengue yaongezeka

Katika hatua nyingine, Wizara imeonya kuhusu hatari ya Homa ya Dengue kufuatia mvua za masika zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini, hali inayochochea mazalia ya mbu aina ya Aedes.

Dk Magembe amesema mbu huyo ni mweusi mwenye madoa meupe na huuma zaidi nyakati za asubuhi, mchana na jioni.

Amezitaja dalili za Dengue ni homa kali, maumivu ya kichwa na viungo, maumivu nyuma ya macho na uchovu, ambazo hufanana na dalili za malaria.

“Natoa rai kwa wananchi kutokomeza mazalia ya mbu kwa kuondoa makopo, matairi na vyombo vinavyoweza kutuama maji, kufukia madimbwi, kuvaa nguo ndefu, kutumia dawa za kufukuza mbu na kuweka nyavu kwenye madirisha,” amesema.

Pia amewataka wananchi kuwahi hospitali wanapopata dalili ili kupatiwa huduma stahiki.

Dk Magembe pia amegusia ugonjwa wa kipindupindu, akisema kwa takribani mwezi mmoja sasa hakuna mgonjwa mpya aliyeripotiwa nchini, baada ya mlipuko uliokuwa umeathiri mikoa yote isipokuwa Kilimanjaro na Njombe.

Mganga Mkuu wa Serikali ametambua mchango wa sekta mbalimbali, taasisi za dini, viongozi wa jamii, wanahabari, sekta binafsi na wadau chini ya usimamizi wa Shirika la Afya Duniani, WHO pamoja na juhudi za wataalamu wa afya katika kudhibiti ugonjwa huo.

Hata hivyo, ameonya kuwa bado kuna hatari ya kurejea kwa ugonjwa huo kutokana na mvua zinazoendelea na uwepo wa maambukizi katika nchi jirani.

“Wananchi wanapaswa kuchemsha au kutibu maji ya kunywa kwa dawa maalumu kama Aquatab au Waterguard, kunawa mikono kwa sabuni kabla ya kula na baada ya kutoka chooni, kuosha matunda kwa maji safi, kuepuka vyakula vilivyoandaliwa katika mazingira yasiyo safi, kujenga na kutumia vyoo bora, pamoja na kutunza mazingira na kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji,” ameonya.

Serikali imeeleza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa magonjwa ya mlipuko na kutoa taarifa mara kwa mara kulingana na mabadiliko ya hali ya maambukizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *