Mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Dodoma Jiji na Simba, imemalizika kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, huku timu hizo zikitoka sare tasa.

Licha ya kutengeneza nafasi nyingi na kushambulia mara kwa mara, Simba ilishindwa kutumbukiza mpira wavuni na kujikuta ikiangusha pointi mbili kwenye mechi hiyo.

Simba iliingia ikiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Dodoma Jiji, kwani mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu, ilishinda mabao 6-0, katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Machi 14, 2025.

Sare ya leo inakuwa ya kwanza kwa Dodoma Jiji dhidi ya Simba, kwani tangu ipande daraja msimu wa 2019-2020, ilikuwa haijashinda wala kutoka sare, zaidi ya kuambulia vichapo kwenye Ligi Kuu.

Tangu Dodoma Jiji ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2020-2021, mechi ya leo ni ya 11, ambapo kati ya hizo imepoteza 10 na kutoka sare moja, huku kikosi hicho cha ‘Walima Zabibu’, kikifunga mabao mawili tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 22.

Matokeo haya, yanaifanya Dodoma Jiji kuendelea kubakia nafasi ya sita na pointi 21, baada ya kucheza mechi 16, ambapo kati ya hizo imeshinda mitano, sare sita na kupoteza mitano, ikifunga mabao 14 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15.

Kwa upande wa Simba inaendelea kubakia nafasi ya tatu na pointi 23, baada ya kikosi hicho kushinda mechi zake saba, sare mbili na kupoteza pia mmoja kati ya 10, iliyocheza, huku ikifunga mabao 18 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne tu.

Baada ya mechi hii, kwa sasa kikosi hicho cha Simba kinajiandaa kupambana na watani zao wa jadi Yanga, katika mechi itakayochezwa Jumapili, Machi Mosi, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *