Mwanga. Wananchi wa Kata ya Kigonigoni, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa mradi wa skimu ya umwagiliaji unaoendelea katika eneo hilo, wakisema kukamilika kwake kutawasaidia kujikwamua kiuchumi na kupunguza umaskini.
Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh16 bilioni na utanufaisha wakulima zaidi ya 24,500 katika kata hiyo, kwa kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao mbalimbali na kuimarisha kipato cha kaya nyingi.
Wakizungumza leo Jumatano Februari 25, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kigonigoni, wananchi hao wamesema wana uhitaji mkubwa wa mradi huo, wakisisitiza kuwa ukikamilika kwa wakati utachochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.
Mkulima wa kata hiyo, Amir Juma amesema kasi ya ujenzi wa mradi huo ni ndogo na kuiomba Serikali kuhakikisha unakamilika kwa muda uliopangwa ili wananchi waweze kuanza kunufaika nao.
“Huu mradi tuliupokea kwa matumaini makubwa kwamba utaleta maendeleo. Tuliambiwa utakamilika Novemba mwaka huu, lakini miezi michache imebaki huku mkandarasi hajatoa matumaini ya kumaliza kazi. Ukikamilika kwa wakati utatusaidia sana sisi wananchi wa kipato cha chini,” amesema Amir.
Naye mkulima Amina Mzirai amesema utegemezi wa kilimo cha mvua ambacho si cha uhakika umekuwa ukiwasababishia mavuno hafifu yasiyokidhi mahitaji ya familia zao.
“Katika vitongoji vyetu hata kuchangia chakula shuleni imekuwa changamoto kwa sababu hatuvuni vya kutosha. Tunategemea mvua ambazo hazitabiriki, hali inayosababisha uhaba wa chakula. Tunaomba mradi huu ukamilike kama ulivyopangwa, maana utatusaidia sana,” amesema Amina.
Baadhi ya wananchi kata ya Kigonigoni, Wilaya ya Mwanga, wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo hilo ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru katika mkutano wa hadhara ambao umefanyika katika Kata ya Kigonigoni, wilayani humo.
Mkulima mwingine, Juma Mdee amesema wananchi wana matumaini makubwa na mradi huo wa umwagiliaji, hivyo ameiomba Serikali kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuleta matokeo chanya kwa wakulima.
Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe amesema anafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo na atahakikisha unakamilika bila vikwazo, akieleza kuwa Serikali imetoa fedha nyingi kugharamia mradi huo kwa lengo la kuwanufaisha wananchi.
Aidha, amewataka wananchi kuwa na subira wakati mkandarasi akiendelea na kazi, akisisitiza kuwa Serikali ipo kazini na haina nia ya kuwakwamisha wananchi.
“Changamoto ya kuchelewa kwa mradi nimeisikia na nitaibeba kama mlivyoiwasilisha. Nitafuatilia katika mamlaka husika na endapo kutakuwa na uzembe wa aina yoyote, tutahakikisha mkandarasi anaongeza kasi ya ujenzi ili mradi ukamilike kwa wakati na wananchi waanze kunufaika,” amesema Dk Maghembe.
Naye Kaimu Mhandisi wa Umwagiliaji Wilaya ya Mwanga, Allan Massepa amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza Mei 2025 na unatarajiwa kukamilika Novemba 2026 kwa gharama ya zaidi ya Sh16 bilioni.
Amesema hadi sasa mradi umefikia asilimia 8.2 ya utekelezaji, huku akitaja changamoto ya kasi ndogo ya mkandarasi kuwa kikwazo kikubwa.
“Mhe. Mbunge, katika mradi huu kuna changamoto ya kasi ndogo ya mkandarasi. Hali hii inawakwaza wakulima ambao huishia kuilaumu Serikali. Tunaomba usaidizi wako katika kulisukuma suala hili ili mkandarasi aongeze kasi na kuwahakikishia wakulima wetu utekelezaji kwa wakati,” amesema Massepa.