Tanga. Wavuvi na wachuuzi wa Soko Kuu la Kasera jijini Tanga wamelalamikia kushuka kwa bei ya samaki na kupungua kwa idadi ya wateja, wakihusisha hali hiyo na kuingiliana kwa vipindi vya mfungo wa Kwaresma na Ramadhani.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Februari 25, 2026, wachuuzi, wavuvi, wanunuzi na wabebaji wa samaki wamesema tangu kuanza kwa mfungo upande wa Wakristo na Waislamu, biashara imekuwa ngumu licha ya samaki kupatikana baharini.
Akizungumza sokoni hapo, mchuuzi Haji Mjaja amesema hali ya biashara siyo nzuri na wala si mbaya sana, lakini kipindi hiki cha mfungo kimeongeza ugumu kwa sababu waumini wa dini zote mbili wako kwenye mfungo.
Wachuuzi na wanunuzi wa samaki wakiendelea na biashara kwenye soko kuu la Samaki Kasera jijini Tanga.
Amesema ndoo ya samaki aina ya Unono iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh150,000 sasa inauzwa kati ya Sh50,000 na Sh70,000 na wakati mwingine hukosa wanunuzi kabisa kwa kuwa hata wauzaji wa rejareja mitaani wanakosa soko.
Mjaja pia ameomba soko hilo liboreshwe na kujengwa kisasa ili kuondoa adha ya kuuzia samaki chini, akisema ni tegemeo kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo ya nje ya mkoa huo.
Kwa upande wake, Rashed Nyange amesema wameathirika kiuchumi kutokana na hali hiyo. Amefafanua kuwa licha ya kutoweka kwa samaki wakubwa, dagaa na samaki wengine wanapatikana, lakini huuzwa kwa shida kwa sababu hakuna wanunuzi.
Mmoja wa wachuuzi wa samaki akipanga mafungu ya dagaa akisubiri wateja kuja kununua katika solo kuu la Samaki Kasera jijini Tanga. Picha Mbonea Herman
Amesema tofauti na zamani, mfungo huo haikuingiliana, safari hii hali imekuwa ngumu zaidi kwa kuwa waumini wa dini zote mbili wanafunga kwa wakati mmoja, hivyo kupunguza walaji.
Naye Ally Juma amesema licha ya kumshukuru Mungu kwa riziki, kwa wafanyabiashara wadogo soko huwa gumu zaidi kipindi hiki kwa kuwa wateja wengi wako kwenye mfungo.
Ameshauri kuanzishwa kwa viwanda vya kuchakata samaki ili kupanua wigo wa soko. Kwa mtazamo wake, uwepo wa soko la viwandani ungewasaidia wavuvi kukabiliana na changamoto za misimu na mifungo badala ya kutegemea walaji moja kwa moja pekee.
Mchuuzi mwingine, Mbwana Said amesema amefanya biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 30 na changamoto kubwa kwa sasa ni kukosekana kwa utaratibu maalumu wa maeneo ya kuuzia kati ya wavuvi na wachuuzi.
Wavuvi wakirejea kutoka habarini wakiwa wamebeba samaki kwenye galoni ikiwa ni kitoweo kwa ajili ya nyumbani kwenye soko la Kasera jijini Tanga. Picha na Mbonea Herman
Amesema zamani mvuvi alipomaliza kuuza samaki wake aliondoka, lakini sasa wavuvi wengi huuza moja kwa moja kwa bei ya chini, hali inayowaathiri wachuuzi kwa kuwa wanashindana katika eneo moja bila mpangilio rasmi.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Wachuuzi wa Samaki, Haji Faki amesema samaki wakubwa wamekuwa adimu katika kipindi hiki, huku dagaa wakipatikana kwa wingi.
Hata hivyo, amesema bei ya dagaa nayo imeshuka kutokana na hali ya hewa, hasa kukosekana kwa jua la kutosha kwa ajili ya kukaushia.
“Ndoo iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh80,000 imeshuka hadi Sh35,000, changamoto kubwa kwa sasa ni uhaba wa samaki wakubwa,” amesema.