Serikali ya Somalia na Umoja wa Mataifa zimetangaza kuwa wananchi wa Somalia wasiopungua milioni 6.5 wanakabiliwa na njaa kali kutokana na ukame ulioiathiri nchi hiyo.

Hali hii ya mambo imeibua wasiwasi siku kadhaa baada ya Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa WFP kutahadharisha kuwa msaada wa chakula unaweza kusitishwa ifikapo Aprili iwapo shirika hilo halitapata uafadhili mpya. 

Somalia ilitangaza hali ya dharura ya ukame mwezi Novemba 2025 baada ya mvua kutonyesha nchini humo kwa miaka kadhaa, huku nchi zingine katika eneo la Pembe ya Afrika pia zikiathirika.

Zaidi ya theluthi moja ya waliokumbwa na njaa kali Somalia ni watoto wadogo. Serikali ya Somalia na Umoja wa Mataifa zimesema katika taarifa yao ya pamoja kwamba mgogoro huu umepelekea makumi ya maelfu ya watu kuhama makazi yao huku wengi wakirundikana katika kambi za wakimbizi katika mji mkuu Mogadishu na katika miji mingine. 

George Conway Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia amesema kuwa ukame umeongezeka katiak kiwango cha kutisha; huku bei ya maji ikipanda,  chakula kikipungua, mifugo inakufa na ufadhili wa misaada ya kibinadamu ukiwa wa kiwango cha chini.

Wiki iliyopita Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ulieleza kuwa watu milioni 4.4 wanatabika na  njaa kali katika na kwamba tayari imepunguza misaada yake kwa zaidi ya watu 600,000 kutoka watu milioni 2.2 mapema mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *