MANYARA: Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Manyara umeendelea kufanya marekebisho ya barabara ya Babati – Singida ili iweze kupitika baada ya kuisha muda wa kipindi cha usanifu wa miaka ishirini.
Kuisha kwa miaka ya kuishi ya barabara hiyo kumetengeneza mashimo makubwa yaliyosababishwa na mafuriko na mvua zinazoendelea kunyesha.
Katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Manyara kilichofanyika ukumbi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mkuu wa Mkoa huo, Queen Sendiga amesisitiza barabara nzuri, miundombinu sahihi ni ukuaji wa uchumi wa mkoa.
”Tunaposema ukuaji wa uchumi ni pamoja na kuwapa elimu wananchi juu ya matumizi bora ya barabara kwa kutopitisha mifugo katika barabara kuu zinazosimamiwa na TANROADS na za mitaa za TARURA , mifugo ipitishwe kwenye njia ya mifugo (mapalio),” amesema Sendiga.
Meneja wa TANROAD, Mkoa wa Manyara, Ndutu Masele amesema barabara hiyo yenye urefu wa km 105 ina kipande kilichoathirika zaidi kwa uwepo wa mashimo cha km 82.
”Changamoto hii inatokea zaidi katika kipindi cha mvua mashimo yanajitokeza kwa wingi, TANROADS inaendelea kuyaziba na kurudisha barabara katika hali yake ya awali,” amesema Masele.
Amesema barabara hiyo kwa sasa inapitisha magari mazito takribani magari mia sita kwa siku yanayobeba mizigo mizito yakitokea bandari ya Tanga na Mombasa kwenda mikoa ya kanda ya ziwa na nchi jirani.
