Mwenendo usioridhisha wa Tanzania Prisons kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, umeufanya uongozi wa timu hiyo leo, Jumatano, Februari 25, 2026 kuachana na Kocha Zedeckia Otieno.
Taarifa ya Tanzania Prisons imesema kuwa mkataba wa kocha huyo umevunjwa baada ya pande mbili kufikia makubaliano.
“Uongozi wa timu ya Tanzania Prisons unapenda kuutaarifu umma kuwa, kwa makubaliano ya pande zote mbili, umefikia makubaliano ya kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Zedeckia Evans Otieno.
“Aidha, Uongozi wa Tanzania Prisons Football Club unamshukuru Kocha Otieno kwa mchango na huduma yake kwa kipindi chote alichoitumikia timu na unamtakia kila la heri katika majukumu yake,” imesema taarifa hiyo.
Aliyekuwa kocha wa Tanzania Prisons, Zedeckia Otieno, ambaye ametimuliwa kwenye Klabu hiyo baada ya mwendelezo mbaya wa matokeo. Picha na Mtandao
Otieno ameiongoza Tanzania Prisons kupata ushindi katika mechi tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya 14 iliyocheza hadi sasa huku ikitoka sare mara tatu na kupoteza mechi nane.
Timu hiyo inashika nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imekusanya pointi 12 ambazo ni nne juu ya zile za KMC inayoshika mkia.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Tanzania Prisons, zinafichua kuwa mrithi wa Otieno atakuwa ni nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa.
Muenendo mzuri wa Transit Camp kwenye Ligi ya Championship msimu huu chini ya Nsajigwa umeonekana kuishawishi Tanzania Prisons kumchukua Kocha huyo.
Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa, ambaye anaifundisha Transit Camp katika ligi ya Championship, anatajwa kuwa mrithi wa Zedeckia Otieno. Picha na Mtandao
Nsajigwa hadi anaondoka Transit Camp, timu hiyo ipo katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ikiwa na pointi 37 ilizovuna kwenye mechi 19.
Leo, uongozi wa Transit Camp umemuaga rasmi Nsajigwa, jambo linalokoleza tetesi za kujiunga kwake na Tanzania Prisons.
“Uongozi wa timu ya Transit Camp unapenda kutoa shukrani za dhati kwa aliekuwa Mocha Mkuu wa timu yetu Shadrack Nsajigwa.
“Rasmi tunatoa mkono wa kwa heri na kumtakia kheri katika majukumu yake mapya. Kitendo bila kupoa,” imesema Transit Camp.