Dodoma. Tathmini iliyofanywa na Serikali kuhusu stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wa darasa la awali hadi la tatu imebaini kuwa stadi ya kuhesabu iko chini ikilinganishwa na stadi za kusoma na kuandika.

Kwa mujibu wa matokeo ya tathmini hiyo, wanafunzi wengi wanafanya vizuri zaidi katika kusoma, ikifuatiwa na kuandika, huku kuhesabu kukionyesha kuwa na changamoto kubwa zaidi.

Akizungumza leo Jumatano, Februari 25, 2026, katika kikao kazi cha wadau wa elimu kilichoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Children in Crossfire (CiC) jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Elimu Msingi katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Abdul Maulid amewataka wataalamu wa elimu kukaa pamoja na kuchambua chanzo cha udhaifu huo.

Amesema masomo yote ya sayansi yanategemea hisabati, hivyo ili kupata wanasayansi mahiri ni lazima somo hilo lieleweke vyema tangu ngazi ya awali.

“Hapa naona kuna madaktari na maprofesa wabobezi wa hisabati. Naomba mkae chini mjue tatizo ni nini mpaka stadi ya kuhesabu inakuwa chini, kisha mtoke na majibu,” amesema Maulid.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wanafunzi kupata chakula shuleni ili kuwawezesha kuelewa wanachofundishwa.

Ameagiza wanafunzi wote wapatiwe chakula huku wale wa madarasa ya awali wakipatiwa uji, akieleza kuwa njaa huathiri umakini wa mtoto darasani.

Amesema watoto hupoteza umakini kwa sekunde chache wanapokuwa darasani, hali inayoweza kupunguzwa kwa kuhakikisha wanapata lishe bora.

“Mwanafunzi akiwa ameshiba atakusikiliza vizuri kuliko akiwa na njaa,” amesisitiza.

Maulid pia amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuweka utaratibu madhubuti wa utoaji chakulashuleni kwa kushirikiana na wadau wa elimu.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Kiduma Mageni amesema ushirikiano kati ya Mkoa wa Dodoma na CiC tangu mwaka 2020 umeleta mafanikio makubwa.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni ujenzi wa madarasa mapya 33 na ukarabati wa mengine 473 ya elimu ya awali.

Amesema kwa sasa wanafunzi wote wanaosajiliwa kufanya mtihani wa darasa la nne wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu. Pia ameeleza kuwa mazingira ya madarasa ya awali yameboreshwa na kuvutia zaidi, jambo lililochangia kuongezeka kwa mahudhurio ya wanafunzi shuleni.

Mageni amesema mkoa huo una matumaini makubwa na kuendelea kwa ushirikiano na CiC, hasa katika awamu mpya ya kuimarisha stadi za kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la awali, la kwanza na la pili Kondoa Mji na Kondoa DC.

Mkurugenzi mkazi wa Shirika lisilo la kiserikali la Children in Crossfire (CiC) Craig Ferla akizungumza kwenye kikao kazi cha wadau wa elimu Jijini Dodoma leo Februari 25, 2026

Amesema kipaumbele cha Mkoa wa Dodoma kwa sasa ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaoandikishwa darasa la kwanza wanadumu hadi darasa la nne.

“Bado tunakabiliwa na changamoto ya mdondoko wa wanafunzi. Wapo wanaoandikishwa darasa la kwanza lakini baadhi yao huacha shule. Hata hivyo, tuna mpango mkakati wa elimu wa miaka mitatu mitatu wa kukabiliana na hali hiyo,” amesema.

Amefafanua kuwa mkazo unawekwa katika kuhakikisha mwanafunzi anapoanza elimu ya msingi anasimamiwa ipasavyo ili ahudhurie masomo na kukamilisha mzunguko wake wa elimu ya msingi, kuanzia awali hadi darasa la sita, kisha kuendelea na elimu ya sekondari hadi kidato cha nne.

Mageni ameongeza kuwa mkoa utaendelea kushirikiana na wadau wa elimu kuimarisha misingi ya elimu ya awali na msingi ili wanafunzi waweze kufurahia shule na kujifunza kwa ufanisi.

Mkurugenzi Mkazi wa CiC, Craig Ferla, amesema mradi wa Mtoto Wetu Tunu Yetu umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la awali hadi la tatu.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa mradi huo, shirika hilo limewafikia zaidi ya watoto 200,000 katika Mkoa wa Dodoma pamoja na walimu zaidi ya 800 wa madarasa ya awali.

Ferla amesema malengo ya shirika hilo ni kuwafikia watoto milioni 75 ifikapo mwaka 2050, idadi ambayo ni kubwa kuliko Watanzania wote waliokuwepo kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *