DAR ES SALAAM; Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limesema litaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kusimamia na kutetea haki, maslahi na ustawi wa wanachama wake, kwa lengo la kuhakikisha mazingira bora ya kazi, mishahara stahiki na heshima kwa wafanyakazi nchini vinaimarishwa.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam Febuari 25 na Saidi Wamba kwa niaba ya Katibu Mkuu wa TUCTA, ambapo amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya vyama vya wafanyakazi na Serikali ni muhimu katika kujenga mahusiano mazuri ya kikazi na kuongeza tija katika maeneo ya kazi.

Amesema TUCTA itaendelea kusimamia masuala ya msingi yanayogusa wafanyakazi, ikiwemo mikataba ya ajira, usalama na afya kazini, pamoja na ustawi wa wafanyakazi katika sekta mbalimbali za umma na binafsi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masuala ya Jinsia kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGE), Nasra Shagi, ameeleza umuhimu wa kuzingatia usawa wa kijinsia mahali pa kazi, akisisitiza kuwa wafanyakazi wanawake wanapaswa kupewa fursa sawa na kulindwa dhidi ya aina zote za unyanyasaji na ubaguzi.

Naye, Mbunge wa Viti Maalum, Bengi Issa, amewataka wafanyakazi ambao bado hawajajiunga na vyama vya wafanyakazi kujiunga mara moja, akieleza kuwa uanachama unaleta nguvu ya pamoja katika kutetea haki na maslahi yao.

Amesema kupitia vyama vya wafanyakazi, wafanyakazi hupata fursa ya kusikilizwa, kushirikishwa katika maamuzi yanayowahusu, pamoja na kupata msaada wa kisheria na kitaaluma pale inapobidi. TUCTA imeeleza kuwa itaendelea kutoa elimu kwa wafanyakazi kuhusu haki zao na wajibu wao, huku ikihimiza mshikamano na uwajibikaji katika maeneo ya kazi kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.