
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, (UNHCR) limetangaza kuwa, ufadhili endelevu na wa uhakika unahitajka ili kuendeleza ulinzi kwa wakimbizi na kusaidia urejeaji na ujumuishaji wa raia wanaorudi nchini Burundi, wakati huu ambapo kambi zinzowahifadhi zinakabiliwa na msongamano mkubwa na uhaba wa huduma muhimu.
Taarifa iliyotolewa na UNHCR mjini Geneva imesema, zaidi ya wakimbizi 90,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamekimbilia Burundi katika miezi mitatu iliyopita.
“Wengi wao wamehifadhiwa katika eneo la wakimbizi la Busuma, ambalo sasa linahifadhi zaidi ya raia wa 66,000 wa DRC waliowasili tangu mwishoni mwa mwaka 2025,” imebainisha taarifa hiyo.
Akizungumza baada ya ziara rasmi aliyofanya nchini humo wiki iliyopita, Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR anayeshughulikia Ulinzi wa Wakimbizi, Ruvendrini Menikdiwela, ameielezea hali mbaya katika eneo hilo, akibainisha uhaba mkubwa wa maji safi, chakula, dawa, makazi na huduma za ulinzi.
Kipindupindu na magonjwa mengine yanayoweza kuzuilika yangali ni tishio kubwa, huku karibu watu 10,000 wakisalia katika vituo vya mpito vyenye miundombinu duni wakisubiri kuhamishiwa Busuma, ambayo tayari imeelemewa.
UNHCR imesema, kati ya dola milioni 35 zinazohitajika mwaka huu kutoa msaada wa kuokoa maisha nchini Burundi, ni asilimia 20 pekee iliyopatikana hadi sasa. Kwa ujumla, Burundi inahifadhi zaidi ya wakimbizi 230,000, wengi wao kutoka DRC.
Shinikizo hilo linaongezeka huku kukiwa pia na wimbi la Warundi wanaorejea kutoka uhamishoni, hasa kutoka Tanzania. Katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka 2026 pekee, zaidi ya Warundi 28,000 wamerejea kutoka Tanzania, idadi inayozidi malengo ya makubaliano ya urejeaji wa hiari yaliyowekwa Novemba 2025 kati ya serikali husika na UNHCR.
Shirika hilo limeeleza wasiwasi wake kuhusu taarifa za ubomoaji wa makazi ya wakimbizi nchini Tanzania wakati wa urejeaji wa kasi wa hivi karibuni, hali iliyowalazimisha baadhi yao kuishi katika vituo vya kuondokea vilivyojaa kupita kiasi…/