
Songwe. Jumla ya vibanda 72 vinavyozunguka Soko la Ichenjezya, wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe, vimefungwa na maofisa mapato wa halmashauri kufuatia mgogoro wa malimbikizo ya kodi ya pango.
Hatua hiyo imeelezwa kuchochewa na madai ya kutolipwa kwa kodi tangu mwaka 2021 katika vibanda hivyo.
Kufungwa kwa vibanda hivyo kumesababisha wafanyabiashara 167 wanaofanyia biashara ndani ya soko hilo, wengi wao wakiwa wauzaji wa mbogamboga na matunda, kugoma kwa kufunga biashara zao wakishinikiza wenzao kufunguliwa.
Mwenyekiti wa Soko la Ichenjezya, Bernad Kabuje, amesema tangu mwaka 2021 hakukuwa na utaratibu rasmi wa ukusanyaji kodi, wala wafanyabiashara hawajawahi kupewa mikataba au namba za malipo kutoka halmashauri.
Akifafanua kuhusu mgomo, Kabuje amesema wafanyabiashara hao 167 wamefunga biashara kwa hiari kuunga mkono wenzao, wakieleza kuwa shughuli zao zinategemeana na kwamba kufungwa kwa vibanda hivyo kunaathiri mzunguko mzima wa biashara katika soko hilo.
Hata hivyo, ameongeza kuwa tayari suala hilo wamelifikisha kwa mkuu wa wilaya, lakini wamepewa majibu ambayo hayatoi suluhu kwa kuambiwa walipe madeni yanayodaiwa ili vibanda vifunguliwe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, amesema kufungwa kwa vibanda hivyo ni sehemu ya operesheni ya kukusanya madeni ya muda mrefu, akibainisha kuwa deni hilo limeathiri hata kufungwa kwa hoja za ukaguzi.
Mbega amesema kilichobainika hadi sasa ni baadhi ya wafanyabiashara waliingia makubaliano binafsi badala ya kufanya mikataba halali na halmashauri, hali iliyochangia mkanganyiko wa malipo ya kodi katika soko hilo.
“Sasa tumeamua kuchukua hatua zaidi ili kuhakikisha madeni yanalipwa, kilichobainika pale ni baadhi ya wafanyabiashara kuingia makubaliano binafsi na kulipa kodi kubwa ya Sh70,000 kwa mwezi badala ya kufanya mikataba halali na halmashauri, ambapo watalipa kodi ya Sh10,000 tu kwa mwezi,” amesema Mbega.