Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), imeivunja rasmi Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania baada ya kubainika kuwa mapungufu makubwa katika usimamizi wa mali na utekelezaji wa majukumu yake.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya ripoti ya ukaguzi maalum ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kubaini kuwa bodi hiyo ilishindwa kusimamia ipasavyo mali na rasilimali za kanisa, pamoja na kutotekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kupokea ripoti ya ukaguzi huo Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi amesema kuvunjwa kwa bodi hiyo ni hatua ya kisheria inayolenga kulinda mali za taasisi na kurejesha nidhamu ya uongozi ndani ya kanisa hilo.
Amesema pia uongozi wa kanisa umepewa siku saba kuwasilisha majina 10 ya waumini watakaopendekezwa kuwa wajumbe wa kamati ya mpito itakayosimamia mali na shughuli za kanisa mpaka bodi mpya itakapoundwa kwa mujibu wa sheria.
Kanyusi amesema ukaguzi huo maalum ulifanywa kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na baadhi ya waumini wa kanisa hilo katika Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu na kwa Msajili wa Jumuiya za Kiraia chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akituhumu ubadhirifu wa mali za kanisa na matumizi mabaya ya madaraka.
#StarTvUpdate

(Feed generated with FetchRSS)