Unguja. Serikali imesema walimu 258 wamepatiwa mafunzo ya elimu jumuishi na walimu wataalamu 92 wameajiriwa kuhakikisha watu wenye ulemavu wakiwemo wanawake wanapata elimu bila vikwazo.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Februari 25, 2026 na Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais, ambaye pia ni Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma wakati akijibu swali la Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Fatma Ramadhan Mohamed.
Swali hilo lilitaka kutambua mipango ya Serikali kuhakikisha kuwa wanawake wenye ulemavu wanapata elimu, afya na ajira bila ya vikwazo.
Akijibu swali hilo, Hamza amesema, kupitia wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzinzibar, imejenga skuli mbili za dakhalia kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa uoni na usikivu iliyopo Jendele kwa Unguja na Pujini kwa upande wa Pemba.
Pia, amesema Serikali imenunua vifaa kwa ajili ya kujifunzia na kusomeshea wanafunzi wenye ulemavu vikiwemo viti mwendo vya chaji 75, viti vya magurudumu mawili 60, mashine za nukta nundu 40, virikodi sauti 15, vifaa vya michezo 340, fimbo nyeupe 40 na shime sikio 35.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiendelea na kikao katika mkutano wa pili wa Baraza la 11 la Wawakilsihi Chukwani Unguja Zanzibar
“Serikali imeajiri walimu wataalamu 92 kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu na walimu 258 wamepatiwa mafunzo ya elimu mjumuisho,” amesema.
Amesema kwa upande wa upatikanaji ajira kwa watu wenye ulemavu amesema Serikali imeendeleza jitihada za kuhakikisha watu wenye ulemavu wakiwemo wanawake wanapata fursa ya ajira nchini.
Pia, amesema Serikali imetoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu katika nafasi za ajira kwa kupunguza vigezo vya uajiri na kuweka utambuzi wa waombaji wenye ulemavu katika mfumo wa uombaji (ZanAjira).
Amesema Serikali imeanzisha programu mbalimbali za kuwawezesha wananchi
kiuchumi kwa kuwapatia mikopo ya 4-4-2 yenye masharti nafuu na isiyo na riba.