Dodoma. Wananchi waishio pembezoni mwa barabara kuu ya Dodoma – Iringa katika kata za Manzase na Fufu wameiomba Serikali kuboresha ujenzi wa barabara hiyo ambayo imekuwa kero wakati wa mvua.

Wananchi hao wamelalamikia athari za mvua zinazokwamisha mawasiliano, kusababisha maji kujaa kwenye makazi yao na kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.

Wakizungumza leo Jumatano Februari 25, 2026 wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, iliyolenga kukagua hali ya barabara kuu ya Dodoma–Iringa, wananchi wamesema mvua ikinyesha hata kidogo, maji hukatiza barabara na kuacha tope zito kwenye makazi yao.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akikagua barabara kuu ya Dodoma kwenda Iringa.

Mkazi wa Fufu, Lucas Mkuya, amesema changamoto kubwa si mafuriko bali kukosekana kwa mitaro na makaravati ya kupitisha maji kwenda maeneo yaliyokusudiwa.

“Hatuwezi kusema ni mafuriko, lakini hatuna njia sahihi za kupitisha maji kwenda kwenye madaraja yaliyotengenezwa, ndiyo maana maji yanarudi kwenye makazi na barabara,” amesema Mkuya.

Akizungumza katika ziara hiyo, Ulega ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha inatafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la maji linaloathiri kipande cha barabara cha Manzase mkoani Dodoma.

Amesema pamoja na kujenga barabara mpya, lakini miundombinu ya awali, eneo hilo mvua ikinyesha kidogo shughuli za barabara husimama na kuleta kero kwa watumiaji.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, akizungumza na wanahabari katika ziara hiyo ambapo ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha inatafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la maji linaloathiri kipande cha barabara cha Manzase mkoani Dodoma.

Amesema barabara ni mhimili wa uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla, hivyo ni wajibu wa Tanroads kuhakikisha miundombinu hiyo inaboreshwa kwa haraka ili kufungua na kuendeleza shughuli za kiuchumi.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dodoma, Zuhura Amani, amesema tayari wamefanya usanifu wa kitaalamu na kubaini uwepo wa makaravati sita, ambapo matatu ni madogo na mengine makubwa, yote yakihitaji kujengwa kwa haraka.

Zuhura amewahakikishia wananchi wa Manzase na Fufu kuwa ukarabati wa miundombinu hiyo utafanyika kwa haraka na kwa namna ambayo haitavuruga shughuli zao za kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *