
Dar es Salaam. Wakati Wizara ya Afya ikitoa tahadhari kwa wananchi kufuatia ongezeko la wagonjwa wa mafua makali na Uviko-19 nchini, wataalamu wa afya wameeleza sababu za kuongezeka kwa maambukizi hayo katika kipindi hiki.
Aidha, wataalamu hao wametaja makundi yaliyo hatarini zaidi na kusisitiza umuhimu wa kupata matibabu stahiki mapema, badala ya kujitibu bila ushauri wa kitaalamu.
Serikali pia imeonya kuhusu hatari ya homa ya dengue kufuatia mvua za masika zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini, hali inayochochea mazalia ya mbu aina ya Aedes.
Tahadhari ya wizara imetolewa leo Jumatano, Februari 25, 2026 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe akisema kuna ongezeko la watu wanaopata mafua na magonjwa mengine yanayohusiana na njia ya hewa, kama homa, kikohozi na baridi, hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya msimu.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wameeleza hali waliyokumbana nayo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, wakifafanua jinsi walivyobanwa na mafua, kifua na homa, huku wengine wakilalamika kuuma kwa viungo vya mwili.
“Achana na mafua na kikohozi, kuna kuuma viungo, baridi fulani isiyo ya kawaida mwilini, joto kupanda na kushuka, mwili kuishiwa nguvu, kichwa kuuma, kupoteza radha ya chakula, haya yote yamenifika ndani ya siku nne nimeteseka,” ameeleza Atupokile Lesbon.
Mama huyo wa watoto wanne, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam, amesema “nimetibu hawa watoto mpaka nimechoka kabisa, wiki ya tatu sasa watoto wanakohoa na mafua yasiyoisha, tena nina kadogo mpaka kanashindwa kunyonya.”
Mkazi wa Kilimanjaro, Paslina John amesema, “Tumeuguza kifua na mafua mimi na mwanangu, tumekunywa dawa na dawa mpaka ikabidi sasa tusubiri neema ya Mungu tu. Nashukuru Mungu sasa tumepata afadhali.”
Katika tamko lake, Dk Magembe amesema takwimu za ufuatiliaji zinaonyesha kuwa kila mwaka kuanzia Novemba hadi Aprili kumekuwa na ongezeko la maambukizi ya mafua makali ya Influenza na Uviko-19, hali inayoshuhudiwa pia katika nchi nyingine duniani.
Ameeleza kuwa magonjwa hayo huenezwa kupitia majimaji yanayotoka kwenye njia ya hewa ya mgonjwa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza na pia kwa kugusa maeneo yaliyochafuliwa.
Amezitaja dalili zake kuwa ni pamoja na homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu.
“Wizara inazitaka jamii kufunika pua na mdomo wanapokohoa au kupiga chafya, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, kuvaa barakoa wanapokuwa na dalili au wakiwa kwenye maeneo yenye msongamano, pamoja na kuzingatia usafi binafsi na wa mazingira,” ameelekeza.
Wataalamu waonya
Kufuatia hali hiyo, wataalamu wa afya wameshauri wananchi kuwahi vituo vya afya kupata matibabu na kuepuka kujitibu kwa antibaotiki bila ushauri wa kitaalamu.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mfumo wa upumuaji, Elisha Osati amesema ikiwa mtu atapata mafua makali, kikohozi au homa ni muhimu kufika kituo cha afya kupata matibabu, akionya kutomeza antibaotiki au kujitibu.
Amesema magonjwa ya mafua makali na Uviko-19 yanayotokea zaidi kipindi hiki cha mvua na msimu wa joto unavyoanza.
“Wakati hali ya hewa inabadilika na wadudu nao wanabadilika wanatengeneza aina mbalimbali za protini zinazowasaidia kuishi, katika mabadiliko hayo wanaweza kuleta madhara kwa watu,” amesema Dk Osati akisisitiza umuhimu wa kujikinga ili kutoambukiza wengine.
Aidha ameyataja makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kupata madhara makubwa ya magonjwa ya hayo ni pamoja na wenye mzio, waliowahi kuugua Uviko19 hapo kabla, wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, watoto wadogo hasa chini ya miaka mitano, wajawazito na watu wenye magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu, pumu, magonjwa ya moyo, figo au saratani.
“Pia, watu wenye kinga dhaifu wakiwemo wanaoishi na VVU pamoja na wahudumu wa afya na wanaoishi katika maeneo yenye msongamano mkubwa wako kwenye hatari zaidi, hivyo wanapaswa kuchukua tahadhari za kinga ikiwemo chanjo, kuvaa barakoa wanapokuwa na dalili na kuzingatia usafi binafsi,” amesema.
Dengue yaongezeka
Katika hatua nyingine, Wizara ya Afya imeonya kuhusu hatari ya Homa ya Dengue kufuatia mvua za masika zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini, hali inayochochea mazalia ya mbu aina ya Aedes.
Dk Magembe amesema mbu huyo ni mweusi mwenye madoa meupe na huuma zaidi nyakati za asubuhi, mchana na jioni.
Amezitaja dalili za dengue ni homa kali, maumivu ya kichwa na viungo, maumivu nyuma ya macho na uchovu, ambazo hufanana na dalili za malaria.
Kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, Dk Magembe amesema kwa takribani mwezi mmoja sasa hakuna mgonjwa mpya aliyeripotiwa nchini, baada ya mlipuko uliokuwa umeathiri mikoa yote isipokuwa Kilimanjaro na Njombe.
Mganga Mkuu wa Serikali ameonya kuwa bado kuna hatari ya kurejea kwa ugonjwa huo kutokana na mvua zinazoendelea na uwepo wa maambukizi katika nchi jirani.
Lichja ya hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Mlipuko nchini, Dk Vida Mmbaga amesema Tanzania imejenga uwezo mkubwa wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.