Tanga. Kamati za Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (Mtakuwa) katika Kata ya Madanga, Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, zimeeleza kukabiliwa na vitisho vya kujeruhiwa kwa mapanga wakati zikitekeleza majukumu ya kushughulikia watuhumiwa wa ukatili wa kijinsia.

Akizungumza leo Jumatano Februari 25, 2026 kwa niaba ya wenyeviti wa kamati hizo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Madanga, Mbwana Gandi amesema baadhi ya watuhumiwa wamekuwa wakitishiwa maisha yao wanapofuatilia kesi za ukatili.

“Tunaposhughulikia matukio ya ukatili kwenye jamii, baadhi ya wahusika hututishia kwa silaha, hasa mapanga. Hali hii inaleta hofu kwa wajumbe wetu na inakatisha tamaa jitihada za kupambana na ukatili,” amesema Gandi.

Amesema changamoto hizo zinaathiri pia mapambano dhidi ya ndoa za utotoni na mimba kwa wanafunzi, ambazo zimekuwa zikichangia watoto wa kike kukatisha masomo.

Hata hivyo, amebainisha kuwapo kwa mafanikio, akisema wananchi wameanza kujitokeza kuripoti matukio ya ukatili badala ya kuyaficha, huku uelewa kuhusu haki za wanawake na watoto ukiongezeka.

Gandi ametoa kauli wakati wa ziara ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alipotembelea Mradi wa Kuharakisha Upandaji na Urejeshaji wa Misitu kwa Maendeleo ya Kaya (ARTHI) wilayani Pangani.

Akizungumzia uhaba wa rasilimali, amesema kamati hizo zinakabiliwa na changamoto ya usafiri kufuatilia kesi, zikiwamo zinazohitaji kufikishwa polisi.

“Ikitokea kesi ya kwenda polisi hatuna usafiri. Tunaomba Serikali ituunge mkono, ikiwemo kutuwezesha miradi ya kiuchumi kwa wanawake ili kupunguza utegemezi unaochangia ukatili wa kijinsia,” amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Ayub Sebabile, amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa mapema wanapobaini viashiria vya ukatili.

“Wananchi msikae na ukatili ndani ya familia au jamii. Toeni taarifa kwa watendaji wa kata, vijiji, viongozi wa dini na vyombo vya dola ili hatua zichukuliwe mara moja,” amesema.

Ameagiza ajenda ya Mtakuwa iwe ya kudumu katika vikao vya Kamati za Maendeleo ya Kata ili kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo hivyo.

Naye Dk Gwajima amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha mpango wa Mtakuwa unaingizwa rasmi kwenye mipango na bajeti za halmashauri.

“Mpango wa Mtakuwa unaelekeza wazi vyanzo vya fedha. Halmashauri hakikisheni mnatengea bajeti na kuuweka kama ajenda ya kudumu. Haiwezekani matukio ya ukatili yaripotiwe mitandaoni halafu viongozi wa eneo husika hawajachukua hatua,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema  mradi wa ARTHI unaotekelezwa kwa ushirikiano wa World Vision, Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Tanzania, unatarajiwa kuleta manufaa ya kudumu kwa wananchi.

Amesema mradi huo wa miaka miwili wenye thamani ya Sh3.5 bilioni unapaswa kuacha matokeo chanya hata baada ya kukamilika mwaka 2026.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa World Vision Tanzania, James Anditi amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali kuimarisha ustawi wa jamii kupitia miradi ya maji, elimu, afya na uwezeshaji wa kiuchumi.

“Tunaamini mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanahitaji ushirikiano wa wadau wote. Tutaendelea kuisaidia Serikali kujenga jamii salama na yenye fursa sawa kwa wanawake na watoto,” amesema.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya miradi hiyo yanategemea ushiriki wa wananchi, akihimiza jamii kuilinda na kuendeleza miradi hata baada ya ufadhili kukamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *