
Dar es Salaam. Yanga imejiweka katika hali nzuri kuelekea mechi dhidi ya Simba Jumapili hii baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, leo Jumatano, Februari 25, 2026.
Ushindi huo pia umeifanya Yanga ipande kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha pointi 28 sawa na JKT Tanzania lakini yenyewe ina utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa ambapo yenyewe utofauti wake ni mabao 25 huku JKT Tanzania ikiwa na utofauti wa mabao matatu.
Katika mechi ya leo, mabao ya Yanga yamepachikwa na Mohamed Hussein, Laurindo Aurelio ‘Depu’, Mudathir Yahya, Prince Dube na Sheikhan Ibrahim.
Mohamed Hussein ndiye alianza kuihakikishia Yanga ushindi katika mechi ya jana baada ya kuipatia bao la kuongoza katika dakika ya saba, akmalizia vyema pasi ya Prince Dube baada ya wachezaji hao pamoja na Duke Abuya kuchezeshana vyema jirani na eneo la hatari la JKT Tanzania.
Bao hilo lilidumu hadi refa Saady Mrope alipopuliza filimbi ya kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili kilianza kwa JKT Tanzania kufanya mabadiliko ya kuwatoa Karim Mfaume, Anuary Kilemile na Mohamed Bakari ambao nafasi zao zilichukuliwa na Najim Maguru, David Brayson na Laurian Makame.
Mabadiliko hayo yalionekana kuidhohofisha zaidi kwani ilijikuta ikishambuliwa mara kwa mara na kuiruhusu Yanga kupata mabao manne katika kipindi hicho cha pili.
Bao la pili lilifungwa na Depu aliyeunganisha vyema kwa kichwa krosi ya Israel Mwenda katika dakika ya 60 na dakika tatu baadaye, Mudathir Yahya akafunga la tatu akimalizia piga nikupige iliyotokea langoni mwa JKT Tanzania.
Dakika ya 84, Prince Dube akafunga la nne akimalizia pasi ya Bubah Jammeh na Shekhan Ibarhim akapigilia msumari wa mwisho katika dakika ya 89 akiunganisha kwa shuti la mguu wa kushoto, pasi ya Mwenda.
Mabadiliko mengine ya JKT Tanzania katika mechi hiyo yalikuwa ni ya kuwatoa Salehe Karabaka na Sospeter Bajana na kuwaingiza Edward Songo na Tepsi Evance na Yanga iliwatoa Allan Okello, Depu, Abuya, Mudathir na Maxi Nzengeli ambao nafasi zao zilichukuliwa na Mohamed Damaro, Emmanuel Mwanengo, Sheikhan na Bubah.