Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amewataka wabunge na wakurugenzi kuwa na ushirikiano katika utekelezaji wa mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo hususani majimbo 50 ya Zanzibar.

Hemed ameitoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 26, 2026 katika mafunzo maalumu ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoka Zanzibar, yaliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Unguja.

Hemed amesema Serikali inalenga kufanya marekebisho ya sheria ya utaratibu na matumizi ya fedha za mfuko huo kwani baadhi ya halmashauri, mabaraza ya miji na manispaa zimeshindwa kuzisimamia vizuri fedha.

Hivyo, amewataka wakurugenzi na wabunge kwa pamoja kufuata sheria zilizowekwa na Serikali ili kutimiza lengo lililokusudiwa.

“Wabunge na wakurugenzi, nataka mfanye kazi kwa umoja ili kuhakikisha mfuko wa kuchochea maendeleo unatumika kwa ufanisi katika ngazi ya jimbo, kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi wenyewe,” amesema. 

Mbali na hilo, amewasihi viongozi kuacha kufanya kazi kwa nidhamu ya woga kwani hakuna ambaye atakaa milele kwenye nafasi zilizopo.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Yussuf Masauni amesema mfuko huo ulianzishwa kwa lengo la kuchochea maendeleo ya majimbo ya uchaguzi ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema, kutokana na makubaliano ya sheria namba 16 ya mwaka 2009 ya mfuko wa maendeleo ya Jimbo, kifungu cha nne (2) cha sheria kinasema msimamizi kwa upande wa Tanzania Bara ni waziri anayehusika na serikali za mitaa na kwa upande wa Zanzibar ni waziri anayehusika na masuala ya Muungano.

“Kuanzia mwaka 2020 hadi 2026, fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo zilizopelekwa Zanzibar ni Sh8.434 bilioni, nikiwa waziri mwenye dhamana, nahitaji mfuko huu uwe sawa,” amesema. 

Masauni amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kupata maoni ya wabunge katika kufanya marekebisho ya sheria ya mfuko huo ili kuboresha utekelezaji wa kuchochea maendeleo.

Amesema kupitia kikao hicho, kitasaidia kuwasilisha hoja zilizobainishwa kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Amesema, kikao hicho kitasaidia kuboresha makosa yaliyoonekana lakini pia kutumia nafasi hiyo kuyarekebisha makosa yanayotokana na sheria hivyo ni wakati wa kupendekeza maboresho husika.

Hivyo, Waziri Masauni amesisitiza kuwa Serikali ipo tayari kusikiliza na kuboresha panapohitajika kwani ndio msingi wa mafanikio ya mfuko huo. 

Akitoa maoni katika mafunzo hayo, Mbunge wa Chumbuni, Salum Ussi Pondeza amesema mfuko wa jimbo umekuwa na mlolongo mkubwa hususani katika upatikanaji wa fedha zinazotolewa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

Amesema kwa kawaida mfuko huo unasimamiwa na mkurugenzi jambo ambalo linasababisha mvutano kati yao kwa kila mmoja kuwa na matakwa yake.

Hivyo, amesema agizo lililotolewa na Makamu wa Rais linaakisi uhalisia baina ya wabunge na wakurugenzi ni vyema kuungana ili kuchochea maendeleo kama ilivyoelekezwa.

“Hii ndio kero kubwa baina wabunge na wakurugenzi namna ya kuutumia mfuko huo uliowekwa kuwasaidia wananchi na tunahitaji kuwa na umoja,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *