WANARIADHA wa kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay, Emmanuel Dinday na Benard Geay, wamerejea nchini wakitokea Korea Kusini walikoshiriki mashindano ya Daegu Marathon yaliyofanyika Februari 22,2026 na kubeba heshima ya taifa.

Nyota hao wote wanatokea timu ya riadha ya Gabriel Geay inayofanya mazoezi katika kambi ya Madunga iliyopo wilayani Babati mkoani Manyara.

Geay ameendelea kuthibitisha ubora baada ya kutetea ubingwa wake, akitumia muda wa 2:08:08, licha ya kuchelewa kwa dakika 2 na sekunde 48 ukilinganisha na rekodi yake ya mwaka jana ya 2:05:20.

Dinday ambaye ni mwanariadha chipukizi, alimaliza nafasi ya tatu kwa muda wa 2:08:16, sekunde nane tu nyuma ya mshindi akiweka muda wake bora binafsi na kuonyesha wazi kuwa kizazi kipya cha Tanzania upande wa riadha kinaibuka kwa kasi.

Kwa upande mwingine, Benard alikimbia marathon yake ya kwanza na kumaliza wa 13, matokeo yaliyompa matumaini makubwa ya kupanda viwango katika mashindano yajayo. Hata hivyo, mwanariadha huyo mwaka jana alivunja rekodi ya taifa ya Kilomita 15 ambayo ilikuwa inashikiliwa na Geay.

Nyota hao sasa wanaungana na wengine kama Benjamin Fernand, Ambrose Ama, Jumanne Mnada, Alphonce Simbu, Josephat Gisemo, Magdalena Shauri, Hamida Nassoro, Cecilia Panga, Daniel Sinda, Mao Hando, Inyasi Sulle na Mathayo Sombi ambao tayari wamefuzu kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika nchini Uningereza, Julai 2026.

Pia ushindi huo unaifanya Tanzania kufikia idadi ya wanariadha wanne ambao wamefanya vizuri mwaka huu hadi sasa kimataifa, wakitangulia Alphonce Simbu aliyemaliza nafasi ya pili Burj2burj Half Marathon na Magdalena Shauri katika mbio za Rak Half Marathon, mbio zote zilifanyika Dubai.

Akizungumza baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Geay amesema ushindani ulikuwa mkali lakini alizingatia kwanza kushinda na sio kuvunja rekodi yake huku akiongeza kuwa anafurahi kuona vijana ambao anawalea katika kambi yake nao wameanza kufanya vizuri.

“Dinday kuwa mshindi wa tatu ni mafanikio makubwa sana kwangu kwa sababu nilimshika mkono akiwa yupo chini kabisa, mimi mwenyewe nikamweka kwenye programu yangu, nikasema ni kijana ambaye nataka nimsaidie ili aweze kutimiza ndoto zake,” amesema Geay.

Naye Dinday amesema alipofikia kwa sasa baada ya mafanikio katika marathoni tatu alizokimbia anaona kuna mwanga zaidi, hivyo atapambana kuhakikisha anaendelea kuiwakilisha nchi vyema kimataifa.

Mdau wa Utalii, Jasmine Kikwete amesema wataendelea kushirikiana na nyota huyo pamoja na wanariadha wengine ili kuhakikisha nchi inatangazika kupitia utalii wa michezo.

“Huu ushindi sio wa Geay peke yake, ni wa taifa na tuzo hii kama nilivyosema kabla ya kurudi, itakuwa maalumu kwa ajili ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na viongozi wote,” amesema Jasmine.

July Lyimo ni Kamishna msaidizi mwandamizi kitengo cha biashara na masoko Hifadhi za Taifa za Tanzania, amempongeza Geay kwa ushindi na kuendelea kuitangaza nchi huku akiongeza wanatambua thamani ya ushindi huo katika kutangaza vivutio vyetu.

Kamishna mwandamizi wa uhifadhi, Lightness Shoo ambaye ni mkuu wa hifadhi ya Arusha, amesema nyota hao wamerudi na ushindi mkubwa na wameitangaza Tanzania vizuri, ambapo pia wametangaza hifadhi ya Arusha kwani ikumbukwe kabla ya kwenda Korea kusini, Geay alipitia hifadhi hiyo na kuahidi ushindi.

Kaimu meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kaskazini, Praygod Godwin, amesema walimwezesha Geay kwenda Korea Kusini kwa sababu anapokwenda kwenye mashindano kama hayo na kushinda anakuwa anatangaza nchi, na anapoitangaza nchi inapata watalii na wawekezaji mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *