Tanga. Wakati maji yakigeuka lulu kwa wakazi wa Mkata Magharibi, wilayani Handeni, mkoani Tanga, kwa Sadick Idd, safari ya kuyafuata imegeuka chanzo cha maumivu na msongo wa mawazo.

Idd anasimulia Januari 21, 2026 alipata ajali alipofuata maji kwenye Bwawa la Sua, akiwa na baiskeli iliyobeba madumu matano.

“Sikuwa na namna tangu Julai 2025 hatuna maji.  Mabwawa yote yamekauka kuanzia la Mkapa hadi la Serikali maarufu Beria, hivyo tunalazimika kwenda mbali kutafuta maji,” anasema.

Anasema siku ya tukio akiwa njiani, pikipiki ya matairi matatu, maarufu Toyo ilimwangukia kichwani, hivyo kumsababishia majeraha.

“Nilijikuta nikiwa chini, damu zinanitoka, nilipofikishwa zahanati walinisafisha wakaniambia niende Hospitali ya Wilaya ya Handeni. Waliniambia kwa uchunguzi wa awali sehemu ya fuvu kwa mbele imepata ufa,” anasimulia.

Bwawa la Mkata maarufu Beria, lililopo Wilaya ya Handeni, jijini Tanga linalosimamiwa na Serikali likiwa limekauka maji kwa kukosekana mvua kwa muda mrefu.

Anasema madaktari walimwelekeza aanze kutibu kidonda kwanza, kisha apelekwe hospitali ya rufaa kwa matibabu zaidi, zikitajwa hospitali za KCMC na ile ya Taifa Muhimbili (MNH).

“Wameniambia gharama ya awali inaweza kufikia Sh300,000, pesa hiyo si rahisi kwangu. Kipato changu ni cha kujitafuta kwa kuuza maji hadi nifikie pesa hiyo nahisi nitakuwa nimeoza, kwa sasa natibu kidonda,” anasema.

Umbali wa kilomita 24

Hassan Shaban na wakazi wengine, wanasema safari ya kwenda na kurudi kufuata maji hufika kilomita 24.

Shaban anasema wanapofika Bwawa la Sua hawaruhusiwi kuingia moja kwa moja, hivyo hulazimika kutumia jenereta kuvuta maji, jambo linaloongeza gharama.

Wakazi wa Mkata wakiwa wamefika eneo la bwawa la Mkata kufuata maji kutokana na kukosekana kwa maji katika maeneo wanayotoka

Anasema jenereta linahitaji mafuta, pia Toyo, hivyo hutumia Sh10,000 kwa siku kufuata maji. Licha ya kupata faida ya Sh30,000 kwa siku lakini bado ni changamoto kwao.

Shaban anasema gharama za maji wanakofuata ni Sh100 kwa dumu, huku pipa la lita 1,000 linagharimu Sh6,000.

“Maji yanatupa riziki lakini kwa sasa yameisha na yaliyopo ni machafu. Kwa sababu ya shida, hakuna namna watu wanatumia vivyo hivyo,” anasema Shaban.

Gharama ya majisafi

Mfanyabiashara wa maji Mkata Mjini, Hassan Issa maarufu Chinga, anasema hufuata maji Tengwe, Kijiji cha Kimange.

Anasema ana madumu 570 ya lita 20 na kila moja husafirishwa kwa Sh200, wapakiaji humtoza Sh17,000 na washushaji Sh20,000. Huuza dumu moja kwa Sh800.

“Maji haya hukaa siku tatu hadi nne, kisha narudi tena kuchota kulingana na biashara ilivyo,” anasema.

Anasema wateja wanaofika eneo lake la biashara wamekuwa na maswali mengi kwani maji yanayouzwa yanatoka maeneo tofauti, hivyo kuwa sababu ya wengine kutoyaamini yanapopangwa barabarani wakidhani ni ya chumvi na yenye tope.

Maji yanayopatikana katika bwawa la Mkata ambayo yanatumiwa na wananchi wa Mkata kwa matumizi ya nyumbani.

“Gharama ya Sh800 kwa dumu imetokana na umbali ninakochukua maji, wale wanaouza Sh600 wanachota kwenye mabwawa ambayo yanakuwa na tope na mengine ni ya chumvi. Mimi nafuata maji mtoni,” anasema.

Chinga anasema shida ya maji katika eneo hilo inatumika kisiasa, kwa kuwa wagombea wa ngazi mbalimbali hufika kuomba kura kwa ahadi ya kutatua kero hiyo lakini haijawahi kutatuliwa.

“Maji ya Mto Wami yamefika Kijiji cha Manga, umbali wa kilomita chache tu kufika Mkata, lakini kwa miaka 14 nipo hapa sijawahi kuona yakifika kwetu zaidi ya kutumika siasa kila siku maelezo ni yaleyale hata uchumi unayumba kwa sababu hakuna maji,” anasema.

Mkazi mwingine, Hafsa Shaaban anasema wanalazimika kutumia maji kidogo kutokana na gharama licha ya kuwa ni machafu.

Mkazi wa Mkata akiwa ametoka kufuata maji eneo la Tengwe.

“Nyumba isiyo na watoto wadogo tunatumia hadi Sh3,000 kwa siku kwa maji. Ufuaji ni changamoto, dumu moja ni Sh600,” anasema.

Anasema uhaba wa maji huwafanya hata wanafunzi kuonekana wachafu.

“Inapotokea mvua imenyesha tunafurahi, lakini kwa muda mrefu ni manyunyu tu viongozi walifika hapa wakaongea vitu vingi lakini ukweli yale ni maneno ambayo tumeyazoea sisi watu wa eneo lote la Mkata,” anasema.

Mabwawa yakauka, yaota nyasi

Ziara ya Mwananchi iliyofanyika Februari 24, 2026 katika mabwawa ya Mkapa na Mkata maarufu Beria imeshuhudia yakiwa yamekauka, majani yakimea na uwepo wa ndege wanaotafuta maji.

Omary Mohamed, mkazi wa Mkata, anasema walitegemea bwawa la Mkapa ambalo limekauka, hivyo wakahamia Beria nako hali ni ile ile, ambako Toyo na magari hayaruhusiwi kufika eneo hilo kwa sasa.

“Tunahangaika, popote tunaposikia maji yanapatikana tunakwenda kwa sababu tunauhitaji,” anasema.

Kauli ya mbunge

Mbunge wa Handeni, Charles Sungura, Februari 13, 2026, wakati Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba, akiwa ziarani mkoani Tanga, aliibua changamoto ya maji jimboni humo.

Alimuomba Waziri Mkuu kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji ili wananchi waanze kunufaika haraka kwa kuwa, Handeni bado inakabiliwa na tatizo sugu la maji.

“Hawawezi kunielewa, ingawa tunazungumza uzinduzi wa umeme, lakini jimbo langu la Handeni tuna changamoto kubwa ya maji, hivyo naomba kuwe na kasi ya miradi na hili nimeongea na wewe pamoja na Waziri Aweso (Jumaa-Waziri wa Maji)” alisema Sungura.

Aweso akijibu changamoto hiyo mbele ya Dk Mwigulu, alisema Serikali imechukua hatua za haraka kumaliza tatizo la maji Mkata na maeneo ya Handeni, akiahidi kuwa, miradi inayoendelea itakamilika kwa wakati kwa kuwa, fedha zipo na hakuna kisingizio.

Kuhusu changamoto ya Mkata, Aweso alisema chanzo kikuu kinachotegemewa ni bwawa la Mkata lililojengwa na Serikali, lakini wakati wa kiangazi hukauka na kusababisha mateso kwa wananchi.

Kutokana na hali hiyo, alisema wizara imeelekeza suluhisho la haraka kwa kuunganisha Mkata na mradi wa maji kutoka Manga, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, kupitia mtandao wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa).

“Maji ya pale Manga tayari yamefika, tumetoa Sh500 milioni ili maji yale yafike Mkata kwa ombi maalumu la mbunge wao, Charles Sungura. Fedha zimetoka na kazi imekamilika,” alisema.

Wafanyabiashara ya maji eneo la Mkata wakienda kufuata maji.

Aliagiza uongozi wa Dawasa kutoka Dar es Salaam kufika Mkata mara moja kuhakikisha maji yanaanza kupatikana.

“Kesho (Februari 14) viongozi watoke Dar es Salaam wafike hapa Mkata, lazima maji yafike na wananchi wapate huduma ya majisafi na salama,” alisisitiza.

Akizungumza na Mwananchi Februari 25, 2026 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Dawasa, Everlasting Lyaro amesema viongozi akiwamo mtendaji mkuu na mkurugenzi wa miundombinu walikwenda Handeni kufanya tathmini.

Amesema baada ya tathmini wameanza ukarabati wa miundombinu ya maji katika Wilaya ya Handeni, hatua inayotarajiwa kumaliza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wakazi na taasisi za kijamii.

“Hatua hiyo imekuja baada ya timu ya wataalamu kutoka Dawasa kufanya tathmini ya kina iliyolenga kufuatilia mwenendo wa miundombinu inayotoa maji kutoka eneo la Tengwe. Tathmini hiyo ilibaini kuwa pampu ya kusukuma maji ilikuwa na hitilafu za kiufundi, hali iliyozuia tangi la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 200,000 kufanya kazi kwa ufanisi,” amesema.

Hili ni bango lililopo njiani kuelekea bwawa la Mkata.

Ukarabati huo amesema umehusisha pia usafi wa mifumo ili kuwezesha maji yanayotoka Mto Wami kutokea Tengwe kupita bila kikwazo kuelekea kwenye vizimba vinane vya usambazaji.

Kuhusu wanufaika, amesema kukamilika kwa kazi hiyo kumeleta matumaini mapya, kwa kuwa, maji sasa yameanza kufika katika maeneo ya kimkakati ikiwamo Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na maeneo ya mnara wa Vodacom.

Amesema shule mbili za sekondari zilizopo mjini Handeni na maeneo yote yanayozizunguka pia zinanufaika kwa upatikanaji wa maji.

Uchimbaji wa visima

Waziri Aweso alisema wizara itatuma timu maalumu ya wataalamu wa maji chini ya ardhi kufanya utafiti na kuanza uchimbaji wa visima virefu katika Kijiji cha Mkata.

“Nitasimamia mwenyewe, tutachimba visima virefu ili wananchi wa Mkata wapate majisafi na salama,” alisema.

Sehemu ya kuhifadhia maji ya bwawa la Mkata ikiwa imekauka.

Kwa Handeni pekee, alisema zimetengwa Sh171 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji utakaohudumia takribani asilimia 75 ya wananchi.

“Mradi huu utachukua nafasi ya ule wa zamani wa HTM uliojengwa tangu miaka ya 1960 na sasa umechakaa, hakuna kisingizio kwa mkandarasi fedha zipo,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *