
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amemuonya Rais wa Marekani Donald Trump dhidi ya kufanya maamuzi yanayotegemea taarifa zisizo sahihi, akisisitiza kuwa Iran haijawahi kutafuta, haitafuti, wala haitawahi kutafuta silaha za nyuklia.
Akizungumza katika kikao na wanaharakati wa kiuchumi ndani ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) siku ya Jumatano, Qalibaf alijibu kauli za hivi karibuni za Trump kuhusu shughuli za nyuklia za Iran ambazo, kwa mujibu wa Tehran, ni za amani.
Katika hotuba yake ya Hali ya Muungano mbele ya Bunge la Marekani, Trump alidai tena kuwa hataruhusu kile alichokiita “mfadhili mkuu wa ugaidi duniani” kupata silaha za nyuklia.
Qalibaf amejibu kwa kusema: “Katika mahojiano ya awali na CNN, nilimwambia rais wa Marekani asifanye uchambuzi usio sahihi kwa kutegemea taarifa za uongo, kisha kufanya maamuzi yasiyo sahihi.”
Amesisitiza kuwa Iran “haijawahi kutafuta, haitafuti, wala haitawahi kutafuta silaha za nyuklia,” huku akiongeza kuwa licha ya msimamo huo wa wazi, Marekani bado “inaendelea kutumia lugha ya vitisho.”
Spika wa Bunge amekosoa madai ya Marekani wakati wa vita vya siku 12, ikiwemo ripoti za kudai kuwa mji wa Mashhad ulikuwa umeanguka. Amelaani pia kuingilia mambo ya ndani ya Iran na upotoshaji wa taarifa unaofanywa na makundi yanayopinga Iran pamoja na Israel, akisema yaliratibu majaribio ya mapinduzi wakati wa machafuko.
Qalibaf ameongeza kuwa Trump mwenyewe aliingilia moja kwa moja machafuko ya hivi karibuni ambapo aliahidi msaada wa Marekani kwa waibua ghasia na fujo.
Ametupilia mbali madai ya Marekani na Israel kuhusu kuwa eti watu 32,000 waliuawa katika machafuko ya hivi karibuni Iran yaliyofadhiliwa na tawala za kigeni. Ameyataja madai hayo kuwa ya uongo na ya kupotosha umma.
Amesema wahusika wa kweli ni magaidi wa zamani waliohusika na zaidi ya mauaji watu 17,000 nchini Iran, yakiwemo mauaji ya maafisa wa ngazi za juu kama rais, waziri mkuu, mkuu wa mahakama, wabunge, na makamanda wa kijeshi.
Spika Qalibaf pia alirejelea kauli ya mjumbe maalum wa Marekani kwa Asia Magharibi, Steve Witkoff, aliyesema kuwa Trump anashangaa kwa nini Iran haijajisalimisha mbele ya matakwa ya Marekani.
Amesema Wamarekani hawajalielewa taifa la Iran na kuongeza kuwa chaguo zote kuhusu Marekani bado ziko mezani, ikiwa ni pamoja na diplomasia yenye heshima na nguvu za kijeshi za kuzuia mashambulizi.