Iran imepinga vikali madai mapya ya Marekani kuhusu shughuli zake za nyuklia na makombora, pamoja na takwimu za waliouawa katika machafuko ya hivi karibuni, ikiyataja kuwa ni “msururu wa uongo mkubwa” huku ikikosoa kampeni iliyoratibiwa ya upotoshaji wa taarifa dhidi yake.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye akaunti yake ya mtandao wa X siku ya Jumatano, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema madai yanayorudiwa mara kwa mara na maafisa wa Marekani pamoja na utawala wa Israel yanategemea uundaji wa makusudi wa uhalisia wa uongo.

Ameandika hivi: “Waongo wa kitaalamu wana ustadi wa kuunda ‘dhana ya ukweli’.”

Amesema: “‘Uongo ukirudiwa mara nyingi sana, hugeuka kuwa ukweli’ na hii ni kanuni ya propaganda iliyoanzishwa na Joseph Goebbels.” Alikuwa akimuashiria waziri wa propaganda wa Ujerumani ya Nazi na mbinu zake za kuunda maoni ya umma.

Baghaei ameongeza kuwa mbinu hiyo sasa inatumiwa kwa utaratibu na utawala wa Marekani pamoja na wanaofaidika na vita wanaouzunguka, hususan utawala wa Israel ambao unatakeleza mauaji ya kimbari, na lengo lao ni kuendeleza kampeni yao ya upotoshaji na taarifa potofu dhidi ya taifa la Iran.

Kauli zake zilifuata matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye katika hotuba yake mbele ya Bunge la Marekani Jumanne alidai kuwa Iran inafanya kazi ya kutengeneza makombora ya masafa marefu yanayoweza kufikia ardhi ya Marekani na kuhatarisha Ulaya pamoja na kambi za kijeshi za Marekani nje ya nchi.

Trump pia alidai kuwa Washington ilikuwa imeionya Tehran dhidi ya kujenga upya mpango wa silaha, hasa silaha za nyuklia, akisisitiza kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ulikuwa umeharibiwa na sasa unaanzishwa upya.

Baghaei ameendelea kujibu matamshi hayo ya Trump kwa kusema: “Chochote wanachodai kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, makombora ya balistiki, au idadi ya waliouawa katika machafuko ya Januari, ni kurudia tu ‘uongo mkubwa’. Hakuna anayepaswa kudanganywa na uwongo huu unaotangazwa waziwazi.”

Haya yanajiri wakati ambapo utawala wa Trump umeongeza kwa kiasi kikubwa zana za  kijeshi katika Asia Magharibi, huku rais huyo wa Marekani akirejea tena vitisho dhidi ya Iran na kuonya juu ya “siku mbaya sana” endapo hakutakuwa na makubaliano katika mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea kati ya pande hizo mbili.

Washington imeendelea na sera yake ya “shinikizo la juu kabisa”, sambamba na kupeleka zana za kijeshi katika eneo hilo, zikiwemo manowari mbili za kubeba ndege, zaidi ya meli kumi za kivita, na idadi kubwa ya ndege za kijeshi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *