KOCHA Mkuu wa Dodoma Jiji, Amani Josiah, amesema suluhu (0-0), iliyoipata timu hiyo juzi dhidi ya Simba ni kutokana na wachezaji wa kikosi hicho cha ‘walima Zabibu’, kufuata vyema maelekezo yake ya kucheza kwa nidhamu kubwa na kwa heshima.

Akizungumza na Mwanaspoti, Josiah, alisema haikuwa mechi rahisi kutokana na jinsi wapinzani wao walivyokuwa wanacheza, ingawa uimara na mkakati mzuri wa wachezaji wa kikosi hicho ulichangia kupata pointi moja, ambayo kwao ni jambo nzuri.

“Sio rahisi kupata pointi moja au tatu hasa unapocheza na timu ambazo zina wachezaji wazuri na wenye uwezo wa kuamua matokeo, kwetu ni jambo zuri kwa sababu limezidi kutuongezea hali ya kujiamini katika mechi zijazo,” alisema Josiah.

Matokeo hayo, yamemfanya Josiah kuandika rekodi ya kocha wa kwanza wa Dodoma Jiji kupata sare katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Simba, kwani tangu kikosi hicho kipande daraja kutokea Ligi ya Championship, kilikuwa hakijawahi kupata sare wala kushinda.

Tangu Dodoma Jiji icheze Ligi Kuu msimu wa 2020-2021, mechi ya juzi ilikuwa ni ya 11, ambapo kati ya hizo imepoteza 10 na kutoa sare mmoja, huku kikosi hicho cha ‘Walima Zabibu’, kikifunga mabao mawili tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 22.

Kwa maana hiyo, Josiah aliyejiunga na timu hiyo Oktoba 16, 2025, anakuwa ni kocha wa kwanza kwa kikosi hicho kuandika rekodi mpya ya kupata sare katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Simba, kwani kabla ya hapo hakuna aliyeweza kufanya hivyo.

Josiah aliyezifundisha Tunduru Korosho, Biashara United ‘Wanajeshi wa Mpakani’, Geita Gold na maafande wa Tanzania Prisons, ameiongoza Dodoma katika mechi 13, ambapo kati ya hizo ameshinda nne, akitoka sare tano na kuchapwa nne.

Kiujumla timu hiyo iliyoanza msimu huu na Kocha, Mrwanda Vincent Mashami, imecheza mechi 16 za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo imeshinda tano, sare sita na kupoteza tano, ikifunga mabao 14 na kuruhusu 15, ikishika nafasi ya sita kwa pointi 21.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *