
Katika juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Kampuni ya Oryx Gas Tanzania imezindua kampeni maalum ya Ramadhan na Kwaresma iitwayo “Pishi la Kibabe inayokwenda sambamba na punguzo la bei ya mtungi wa gesi wa kilo sita.
Akizungumza leo Februari 20, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo Meneja Masoko na Mauzo wa Oryx Gas Tanzania Shaban Fundi amesema huu ni mwezi wa kujitafakari, kushirikiana, kujitolea na zaidi ya yote kuunganisha watu wote.
“Ili kuunga mkono wateja wetu katika kipindi hiki maalum tunatoa bei ya promosheni kwenye mitungi yetu mipya ya kilo sita itauzwa kwa Sh37,000 nchi nzima hadi Zanzibar.”amesema Fundi
Pia wateja wao watakaonunua au kujaza gesi kwenye maduka maalum ya Oryx na Mangi Shop watapokea zawadi ya futari papo kama ishara ya shukrani yao kwao.
Akizungumza kuhusu gharama za mtungi wa kilo sita amesema mpaka unafika nchini Tanzania gharama yake haipungui Sh80,000 lakini Oryx katika soko mtungi huo unapatikana kwa Sh40,000 na kwa sasa tumetoa promosheni mpaka Sh37,000.
“Kuhusu gharama ukilinganisha mkaa na kuni bei yake iko juu zaidi ya nishati safi ya kupikia kwani kwa familia ya kawaida kwa siku moja inatumia kopo moja la mkaa ambalo linauzwa Sh2000 hivyo kwa mwezi ni Sh60,000 wakati mtungi wa gesi ya oryx wa kilo 6 ni Sh40,000.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amesema lengo la kampeni iliyozinduliwa kwa ajili ya Mfungo wa Mwezi wa Ramadhan na Kwaresma ni muendelezo wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.
“Oryx Gas lengo letu kubwa ni kuendelea kuhamasisha nishati safi ya kupikia na mimi na timu yangu tumejipanga vema kuhakikisha tunaendelea kufanya kampeni za kuwezesha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.Wakati huu wa Ramadhan na Kwaresma tunawatakia mfungo mwema lakini wakati huo huo tukihamasisha matumizi ya nishati safi.”
Wakati huo huo Mkuu wa Idara ya Mauzo ya Gesi kwa Ujumla Carloline Msokwa amesema kipindi hiki Waislamu na Wakristo wanaungana pamoja kuomba toba na ni kipindi ambacho familia zinakaa kufanya ibada na kuomba toba lakini pia ni wakati wa kupika chakula kizuri kwa ajili ya kufuturu.
“Kwa hiyo Oryx Gas tumekuja na kampeni ya Pishi la kibabe ambapo familia zitakaa na kupika pamoja lakini pia Oryx tumetoa punguzo la bei ili kuwezesha wananchi kutumia gesi.”