Serikali imesisitiza kuwa mfumo wa stakabadhi za ghala ni muhimu na kichochezi kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Huku ikiendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kunafanyika urasimishaji wa bidhaa za Tanzania kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala, ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kulinda masilahi ya wakulima, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha uchumi wa nchi.
Hayo yameelezwa jana Februari 25,2026 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga wakati wa kufunga msimu wa matumizi ya mfumo wa stakabadhi za ghala msimu wa 2025/2026 na kufungua msimu mpya wa 2026/2027,hafla iliofanyika mkoani Simiyu.
Kapinga alisema mfumo wa stakabadhi za ghala unatekelezwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,kwani mfumo huo unatoa mchango wa moja kwa moja katika kutekeleza dira hiyo.
Kupitia mfumo huo wanakuza uchumi shindani, ushindani katika soko, kukuza mapato ya wananchi na kupunguza umaskini, kuimarisha upatikanaji wa mitaji na huduma za kifedha vijijini.
Pia kuchochea mageuzi ya kilimo na biashara za mazao, kukuza viwanda na mnyororo wa thamani, kuimarisha utawala bora na uwajibikaji, kukuza mifumo ya Tehama na matumizi ya kidijitali, kuimarisha nafasi ya vijana na wanawake katika uchumi, kuchangia usalama wa chakula pamoja na kudhibiti upotevu wa mazao baada ya mavuno.
“Nasisitiza kuwa msimamo wa Serikali na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na ilani ya CCM, (Chama cha Mapinduzi) kwamba stakabadhi za ghala ni ulinzi wa wakulima.”
“Mara kadhaa Rais amekuwa akisisitiza na kuelekeza kuwa mauzo ya mazao lazima yaendane na bei ya soko na siyo shinikizo la nje ya soko halisi, mfumo lazima uzingatie haki, uwazi, kulipa kwa wakati na kuzuia ubadhilifu,”alisema Kapinga.
Sanjari na hayo Kapinga alisema kutokana na upanuzi wa mfumo wa stakabadhi za ghala katika maeneo mapya na ongezeko la mazao yanayouzwa kupitia mfumo huo, bado kumekuwepo na changamoto ya uelewa mdogo miongoni mwa wadau katika baadhi ya maeneo.
“Ninaielekeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB),kutoa elimu kwa wadau wa sekta mbalimbali na kuhakikisha mfumo unatekelezwa kwa ufanisi,”alisema Kapinga.
Pia alisisitiza kuwa mkazo uwekwe katika utoaji wa mafunzo na uhamasishaji kwa wakulima, wafanyabiashara, wasimamizi wa ghala, na wadau wengine muhimu ili kuongeza uelewa na kuboresha ushiriki wao katika mfumo huo.
“Bodi ihakikishe wale wenye maghala ambayo hayajakidhi vigezo, wanawezeshwa ili wafanikiwe kutoa huduma bora na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa mfumo huo.”
Mkurugenzi wa WRRB, Asangye Bangu alisema kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala katika msimu wa 2025/2026,zaidi ya tani milioni 1.1 za mazao zilikusanywa na kuuzwa ikiwa ni ongezeko la asilimia 43 ikilinganishwa na msimu wa mwaka 2024/2025.
Alisema mbali na hilo, wakulima walilipwa takribani Sh2.4 trilioni kupitia mauzo hayo na mazao yalioongoza ni pamoja na korosho tani 439,088 asilimia 39 kwa mikoa ya Morogoro, Singida, Pwani, Lindi, Mtwara,Ruvuma, Tanga na Mbeya.
“Mbaazi tani 270,739 sawa na asilimia 25 kwa mikoa ya Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma,Manyara, Katavi na Rukwa. Ufuta tani 221,603 sawa na asilimia 19 kwa mikoa ya Morogoro, Pwani, Lindi, Ruvuma, Iringa, Songwe, Katavi na Rukwa,”alisema.
Alisema mbali na hayo pia ajira rasmi 1,430 zilipatikana katika maghala huku zaidi ya ajira 10,000 zisizo rasmi zilipatikana na kwa sehemu kubwa ni vijana huku halmashauri zilipata takribani Sh65 bilioni kama ushuru.
“Maghala 286 yalipatiwa leseni ikiwa ni ongezeko la asilimia 19 kutokana na kutanuka kwa matumizi
ya mfumo, idadi ya waweka mali iliongezeka kutoka 224 hadi 788 sawa na ongezeko la asilimia 25,hii ni kutokana na mikoa ya Kanda Ziwa kutekeleza mfumo huo. Wilaya zinazotumia mfumo zimeongezeka kutoka 65 msimu wa 2024/2025
hadi 114 2025/2026,”alisema.
Pia alisema kuna changamoto ya uhaba wa maghala bora hivyo wanahimiza sekta binafsi na halmashauri kuwekeza katika ujenzi wa maghala ya kisasa.
Alisema katika msimu wa 2026/2027,bodi hiyo itaweka mkazo katika kuimarisha matumizi ya Tehama kupitia mfumo wa WRS-MIS, kupanua matumizi ya meneja dhamana katika bidhaa za nafaka na mafuta.
Pia kuratibu rasmi ushiriki wa sekta ya mifugo, ngozi na mwani pamoja na kutoa elimu kwa wakulima, vyama vya ushirika na wakusanyaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha alisema kufunga na kufungua msimu wa mauzo ya mazao katika Mkoa huo kumekuwa chachu na hamasa kwa wananchi kwani wameelewa maana na faida za kuendelea kutumia mfumo huo.
Mmoja wa wakulima wa Mkoa wa Simiyu, Mariam Litwina alisema wakulima wananufaika na mfumo wa stakabadhi za ghala, kwa kuuza mazao yao katika mnada kwa uwazi kwa bei nzuri na kupata fedha kwa wakati.
Kwa upande wa wafanyabiashara mkoani humo akiwamo Daud Mpina alisema kupitia mfumo huo wanapata soko la uhakika na wateja kutoka nje ya mkoa huo kwa urahisi, huku akiiomba Serikali kuendelea kuboresha mfumo huo.