HOSPITALI nchini Kenya zinakabiliwa na ongezeko la mzigo wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza hali inayoongeza changamoto katika utoaji wa huduma za afya. Katika hospitali za umma, watoto wanaolazwa kwa malaria au animonia huonekana pamoja na wagonjwa wa kiharusi, kisukari na saratani, magonjwa ambayo sasa yanaongezeka tofauti na ilivyokuwa awali.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Uchambuzi wa Hali ya Idadi ya Watu ya mwaka 2025, magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo, kisukari, saratani na matatizo ya afya ya akili yanachangia karibu asilimia 40 ya vifo vyote nchini humo.
Hata hivyo, magonjwa ya kuambukiza kama malaria, kifua kikuu na VVU bado yanaendelea kuathiri wananchi wengi, hali inayolazimisha sekta ya afya kupambana na changamoto mbili kwa wakati mmoja. Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Idadi ya Watu na Maendeleo, Dk Mohamed Sheikh amesema ripoti hiyo ni onyo kuwa vifo vingi vinavyotokea vinaweza kuzuilika iwapo huduma za afya zitaimarishwa.

Aidha, kiwango cha vifo vya wajawazito bado ni kikubwa, kikiwa vifo 355 kwa kila vizazi hai 100,000, huku wanawake wa maeneo ya Mandera na Wajir wakikabiliwa na hatari zaidi kutokana na uhaba wa wahudumu na huduma za afya. SOMA: Presha ya uchumi yatikisa Kenya 2027
Ripoti pia inaeleza kuwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano bado vinachangiwa na matatizo ya kuzaliwa, kuzaliwa kabla ya wakati, nimonia, kuhara na utapiamlo, licha ya kuwepo kwa tiba nafuu. Hali hiyo inachangiwa pia na upungufu wa madaktari, wauguzi pamoja na uhaba wa dawa katika baadhi ya maeneo.
Wakati huohuo, ongezeko la idadi ya watu linaendelea kuongeza shinikizo katika mfumo wa afya, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wako chini ya miaka 25. Wataalamu wa afya wanashauri serikali kuimarisha huduma za msingi, kuongeza upatikanaji wa dawa na uzazi wa mpango pamoja na kuboresha mazingira ya kazi kwa wahudumu wa afya ili kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.