DAR ES SALAAM: KATIBU Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhinte, amesema ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha maendeleo jumuishi, akisisitiza kuwa makundi maalum yanapaswa kuwezeshwa kwa kupatiwa mahitaji yao muhimu ili kuhakikisha hakuna mtu anayebaki nyuma katika safari ya ujenzi wa taifa.

Mhinte amesema hayo leo Februari 26, jijini humo wakati wa kupokea msaada wa vifaa saidizi na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 40 kwa ajili ya hospitali za wilaya na rufaa za mkoa huo.

Amesema msaada huo una manufaa makubwa kwa wananchi na ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya uchumi jumuishi inayolenga kuwainua wananchi wote bila ubaguzi.

Ameongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha sekta ya afya na kuboresha huduma za kijamii, hasa kwa makundi yenye uhitaji maalumu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa GSM Foundation, Faith Gugu, amesema taasisi hiyo imetoa msaada huo kama sehemu ya kurejesha kwa jamii.

Ameeleza kuwa vifaa hivyo vitapelekwa katika hospitali sita za Dar es Salaam pamoja na Chama cha Watu wenye Ualbino na Chama cha Wasioona, kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma na kusaidia makundi hayo kuishi kwa urahisi zaidi.

Naye, Katibu wa Chama cha Watu wenye Ualbino Mkoa wa Dar es Salaam, Gaston Mcheka, ameishukuru taasisi hiyo kwa msaada huo akisema utasaidia kupunguza changamoto wanazokumbana nazo katika kupata huduma muhimu.

Aidha, Katibu wa Chama cha Wasioona Mkoa wa Dar es Salaam, Honorati Ngowi, amesema msaada huo ni faraja kwa wanachama wao na utaongeza uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *