MASHABIKI wa Yanga wanachekelea ushindi wa timu yao wa mabao 5-0 dhidi ya JKT Tanzania, huku wenzao wa Simba wakinuna baada ya suluhu 0-0 mbele ya Dodoma Jiji, lakini baadhi ya wadau wamesema matokeo hayo hayatoi picha ya matokeo ya Dabi ya Kariakoo kutokana na ukweli mechi za watani huwa zina matokeo ya kushangaza.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na baadhi ya makocha na wachezaji wa timu mbili za mwisho zilizocheza na miamba hao wa soka nchini na kuna mambo muhimu wameyasema.
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema matokeo ya Simba na Yanga katika mechi mbili za mwisho kabla hazijakutana katika dabi ya Machi Mosi, hayatafsiri chochote bali anaona itakuwa mechi ya kushangaza na haitazidi mabao mawili.
“Maandalizi ya dabi ni tofauti, haijalishi timu mojawapo inaweza ikafungwa ama kutoka sare mechi tatu mfululizo, zinapokutana zinaonyeshana ushindani wa juu,” amesema kocha Ally na kuongeza;
“Kwa upande wangu naona eneo la mabeki ndilo litakaloamua matokeo. Nimeona katika mechi, mipira inayoanza kwa mabeki haikai sana kwa viungo inapitiliza kwa washambuliaji na hazijaruhusu mabao mengi, ndiyo maana nasema haitakuwa mechi ya mabao mengi yanayozidi mawili.
“Yanga ina mabeki wa kati waliokaa pamoja kwa muda mrefu, Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Simba baada kuumia kwa Willson Nangu beki aliyesajiliwa dirisha dogo, Ismail Toure anafanya kazi nzuri na Rushine De Reuck pia zimesajili wachezaji wazuri ambao unaona wataibua ushindani mkali.”
Kwa upande wa kipa wa Tanzania Prisons, Musa Mbisa amesema: “Kwa namna zinavyocheza Simba na Yanga katika mechi za hivi karibuni, zina wafungaji wazuri na ngumu kuzifunga, hilo litachangia mechi yao kuwa ngumu na ushindani mkali.”
Nahodha wa Namungo, Jacob Masawe amesema: “Simba na Yanga ni watani wa jadi, zinapokutana zinakuwa na nguvu tofauti na zinapocheza na timu nyingine, binafsi naiona itakuwa dabi ngumu, haijalishi matokeo ya mechi zao zilizopita hivi karibuni.”
Mechi mbili za Simba na Yanga kabla ya kukutana kwenye Uwanja Amaan Complex, Zanzibar, vijana wa Jangwani wamekusanya pointi sita na mabao sita, wakati Msimbazi imekusanya pointi nne na mabao mawili kupitia mechi zilizopita ndani ya wiki iliyopita.
Mechi hizo ni Namungo 0-1 Yanga iliyochezwa Feb, 22 kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi mfungaji wa bao akiwa ni Laurindo Dilson Depu na kisha mechi ya Yanga 5-0 JKT Tanzania, iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC, Feb 25, wafungaji wakiwa ni Mohamed Hussein Zimbwe Jr, Depu, Mudathir Yahya, Prince Dube na Shekhan Ibrahim.
Mtani wake wa jadi alishinda dhidi ya Tanzania Prisons 2-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Feb 22, wafungaji wakiwa ni Selemani Mwalimu na Rushine De Reuck na Dodoma Jiji 0-0 Simba, iliyopigwa juzi Jumatano.