Mbeya. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Mbeya unakusudia kufanya tathmini ili kupata taarifa za kaya za makundi maalumu ambayo hayajasajiliwa kwenye Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuwekwa kwenye utaratibu wa awamu ya pili.

Mkoa wa  Mbeya unatakiwa kusajili kaya 33,362 lakini mpaka sasa wamezifikia kaya 9,740 sawa na asilimia 33 huku lengo likiwa ni kuhakikisha walengwa wote wanafikiwa na kusajiliwa katika mpango huo.

Miongoni mwa sababu ni pamoja na baadhi ya kaya kuhama, kuolewa na wengine kwenda masomoni, jambo ambalo linalowalazimu baada ya kuhitimisha shughuli hiyo kufanya tathimini kubaini changamoto.

Takwimu hizo  zimetolewa jana Februari 25,2026 na Msimamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Mbeya, Nicolaus Mwangomo, wakati wa mafunzo ya kutoa elimu kwa makundi ya watu wenye ulemavu kujua manufaa ya kujiunga na mfuko huo. Mafunzo hayo yaliratibiwa na Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH).

Mwangomo amesema elimu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu ya kuwekeza nguvu kwenye mkakati wa bima ya afya kwa wote, ndani ya siku 100 tangu achaguliwe kuongoza Taifa.

“Kwa sasa tunaendelea kupokea majina ya kaya ambazo zimetambuliwa na mamlaka husika na kulipiwa michango yao kutoka serikalini kupitia hazina,” amesema.

Mwangomo amesema kwa sasa usajili upo hatua za mwishoni ambapo wanatarajia kuhitimishwa wiki ijayo sambamba na kufanya tathmini ili kujua idadi ya kaya zilizosajiliwa na wasiosajiliwa ili kuziweka kwenye utaratibu wa awamu ya pili.

“Tulitakiwa kusajili kaya 33,000 kwa Mkoa wa Mbeya, lakini mpaka sasa zimesajiliwa 9,740, lakini tumebaini sababu mbalimbali ikiwepo kuhama makazi, kuolewa na wengine kwenda masomoni,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk Godlove Mbwanji amesema Serikali imeona umuhimu wa mpango wa bima ya afya kwa wote na ndio lengo la kupitia sheria kwa kuanzia usajili kwa makundi maalumu.

“Tumeona pamoja na makundi mengine yote tupate angalau washiriki katika mafunzo haya ili kuwa mabalozi kwa wengine, lengo ni kuhakikisha makundi maalumu yakipewa kipaumbele,” amesema.

Baadhi ya watu wenye ulemavu walio shiriki mafunzo ya umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote. Picha na Hawa Mathias

Kauli ya wenye walemavu

Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Mkoa wa Mbeya, Tusajigwe Mwalwega amesema wana kila sababu kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na uongozi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kutoa fursa ya kuwapa elimu kuhusiana na umuhimu wa kuwa mpango huo, jambo ambalo awali waliona kama ndoto.

Naye, Mwenyekiti Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata) Mkoa wa Mbeya, Lucas Mahengea amesema imekuwa fursa kubwa kupata elimu ya kujiunga na mpango huo, jambo ambalo litakuwa neema kutokana na changamoto wanazokumbana nazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *