Dar es Salaam. Siku tisa zikiwa zimepita tangu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kutawatangazia wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao maeneo yasiyo rasmi kuondoka, baadhi ya maeneo yameonekana kuanza kupitika kwa sasa tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma.
Baadhi ya barabara ambazo zimeanza kupitika ni pamoja na ya Mtaa wa Tandamti, Mkunguni na Nyamwezi yote ikiwa ya kuelekea Soko Kuu la Kariakoo ambapo wananchi wanaopita maeneo hayo wameonekana kufurahishwa na hali ilivyo.
Sambamba na hilo, kumekuwa na urahisi wa vyombo vya moto yakiwemo magari, bajaji kuingia na kutoka bila sokoni humo bila bughdha.
Februari 8, 2026, katika hafla ya ufunguzi wa Soko Kuu la Kariakoo, iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema kuanza huduma katika Soko Kuu la Kariakoo kutaambatana na kufunguliwa na barabara zote zinazoingia na kutoka sokoni humo.
Hatua hiyo kwa mujibu wa Chalamila, inalenga kuongeza usalama wa soko hilo, urahisi wa huduma na kurahisisha uokozi inapotokea changamoto.
Alisema tayari ameshazungumza na wafanyabiashara wote kuanzia sasa barabara zote ndani ya soko hilo zitafunguliwa, ingawa anafahamu maelekezo hayo yanaweza kuwa machungu kwa baadhi ya watu.
Katika kulitekeleza hilo, Jumanne Februari 17, 2026 maeneo mbalimbali ya Kariakoo kulikuwa kumebandikwa matangazo ya kuwataka wafanyabiashara waliopo maeneo yasiyo rasmi kuondoka.
Tangazo hilo lililosainiwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya ilitaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na katikati ya barabara za mitaa na njia za waenda kwa miguu, ambao hawajapangwa waondoe bidhaa zao mara moja.
Mbali na wafanyabiashara pia tangazo hilo liliwagusa waendesha bodaboda na bajaji ambao imeelezwa watapaki katika maeneo ya vituo rasmi na wale wasio na vituo watapewa mwongozo na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji hilo.
Hali ilivyo katika Soko la Kariakoo.
Kwa upande wa magari yote ya kushusha na kupakia mizigo yenye vibali vya kuingia mjini, tangazo hilo lilieleza kuwa yataruhusiwa kuingia maeneo ya mjini kuanzia saa mbili kamili usiku hadi saa mbili kamili asubuhi, huku atakayebaikia hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha kwa wafanyabiashara wote wenye maduka wanatakiwa kuondoa bidhaa zote zilizopo nje ya maduka yao kinyume na taratibu za biashara.
Hali ilivyo sasa
Mwananchi jana Jumatano Februari 25, 2026, ilipita katika baadhi ya barabara zinazoingia sokoni humo na kuzikuta zikiwa wazi tofauti na zamani ambapo wafanyabiashara walipanga bidhaa zao hadi katikati ya barabara.
Pia baadhi ya mitaa ilishuhudia Mgambo wakiwa wanazozana na wafanyabiashara ambao wanakaidi amri ya kutokuwepo maeneo hayo.
Hata hivyo, suala la magari ya mizigo kuingia mchana katika maeneo hayo, waendesha bajaji na bodaboda, limeonekana bado kuwa mfupa mgumu kwani wameendelea na shughuli zao kama kawaida.
Anna Lema, mkazi wa Kimara, aliyefika kufanya manunuzi sokoni hapo alisema amefurahishwa na namna barabara zinavyopitika kwa urahisi na kueleza anatamani hali hiyo iwe kwa Kariakoo nzima.
Naye Michi Athumani alisema ana wasiwasi kama hali hiyo itakuwa ya kudumu kwa kuwa kuna wakati wafanyabiashara hao ni kama wanawavizia Mgambo wanaosimamia kuwaondoa katika maeneo hayo, wakiondoka wanarudi na kupanga bidhaa zao.
“Mie ushauri wangu nadhani nguvu ya Mgambo iongozwe, lakini pia wawepo saa 24 ili maeneo hayo yaweze kuwa wazi nyakati zote, kwani ikishafika saa kumi jioni wafanyabiashara wengi wanarejea barabarani,” amesema.
Wakati wananchi wakisema hivyo kwa upande wao wafanyabiashara, Zuhura Omar, alikiri ni kweli kuanzia saa kumi huwa wanarejea barabarani, lakini kwao inawawia vigumu kufanya biashara.
“Saa kumi jioni, muda huo ndio watu wanarejea majumbani utamuuzia nani, ndio maana mchana tupo radhi kukimbizana na Mgambo ilimradi nasi tupate chochote kitu cha kwenda kula na familia zetu.”
Akizungumzia hali hiyo, Makamu Mwenyekiti wa wamachinga Taifa, Steven Lusinde alisema shughuli ya kuwaondoa wafanyabiashara waliokuwepo kwenye maeneo yasiyo rasmi, haikuwa ndogo ukizingatia ni eneo ambalo wanajipatia riziki yao ya kila siku.
Hata hivyo, wakati maelekezo yanatolewa ilikuwa kuondolewa kwa waliokuwa hawajapangwa, Lusinde alisema kwa bahati mbaya limewagusa zaidi ya wafanyabiashara 400 waliokuwa wamepangwa katika maeneo mbalimbali na hivi sasa wanachosubiri ni kupatiwa maeneo mbadala.
Aliyataja maeneo ambayo wafanyabiashara hao walikuwa wamepangwa kihalali ni pamoja Mtaa wa Pemba na Nyamwezi, Pemba na Msimbazi, Tandamti na Swahili, Tandamti na Msimbazi.
Wakati maeneo ambayo watu wamevamia ni pamoja na Mtaa wa Nyamwezi na Mkunguni, Nyamwezi na Tandamti, Mkunguni na Msimbazi na Mkunguni na Tandamti.
Akilizungumzia hilo,Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alikiri wamewaondoa baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wamepangwa na kueleza kuwa wapo katika mchakato wa kuwatafutia maeneo mbadala yakiwemo yaliyopendekezwa na wafanyabiashara wenyewe.
“Ni kweli shughuli ya kufungua barabara imewagusa na waliokuwa wamepangwa kihalali, lakini niwaombe wawe na subira wakati tukiangalia maeneo mbadala ya kuwapeleka,” alisema Mpogolo.
Kuhusu maeneo mengine kusalia kuwa na wafanyabiashara, Mkuu huyo wa Wilaya alisema wamejipa wiki mbili kwa ajili ya kutoa elimu ili hatua za kuwaondoa zitakapoanza kuchukuliwa kusiwe na wa kumlaumu na kueleza hadi sasa imebaki wiki moja tangu tangazo la kuwataka waondoke kwa hiari lilipotolewa.