
Arusha. Ili kuboresha shughuli za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, mradi maalumu wa kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wazalishaji na wafanyabiashara wadogo wa Wilaya ya Karatu na Monduli, umezinduliwa.
Mradi huo umelenga kuongeza urejeshaji wa misitu, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, uhakika wa chakula na kuongeza mitaji kwa wazalishaji na wafanyabiashara hao. Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Februari 26, 2026 Mratibu wa Mtandao wa Wakulima na Wafugaji Mkoa wa Arusha (Mviwaarusha, Richard Masandika, wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kimataifa wa Forest and Landscape Restoration Initiative (FR100) unaolenga kurejesha hekta milioni 100 za mazingira barani Afrika.
Amesema mradi utawezesha kuongeza urejeshaji wa misitu, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, uhakika wa chakula ambayo kwa kiasi kikubwa unachangiwa na shughuli za kibinadamu.
Amesema kwa upande wa Arusha, mradi huo unaoanza katika wilaya hizo mbili wamejipanga kurejesha hekta 70,000 za misitu kupitia ushiriki wa jamii na vikundi mbalimbali, ikiwemo vikundi vya kifedha vitakavyosaidia wanachama kupata mitaji ya kuendesha shughuli za uhifadhi na uzalishaji endelevu.
“Katika kufanikisha hilo, kutakuwa na mfuko maalumu utakaoshirikisha taasisi za kifedha na mashirika ya wawezeshaji kwa lengo la kujenga uwezo wa vikundi vya kifedha na kuhakikisha wazalishaji wadogo wanapata mitaji ya moja kwa moja,” amesema Masandika.
Amesema utekelezaji unafanyika ngazi ya vijiji kwa ushirikiano na vikundi vya Monduli na Karatu pamoja na halmashauri za wilaya husika ili kuwafikia walengwa moja kwa moja.
Awali, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkuu wa Chuo cha Misitu Olmotony, Dk Joseph Makero amesema Serikali ina matumaini makubwa na mradi huo ambao kupitia mfuko maalumu utaondoa changamoto za muda mrefu zinazowakabili wazalishaji wa mazao ya misitu.
Amesema kwa miaka mingi, wazalishaji wa misitu wamekuwa wakikosa mikopo kutokana na mzunguko mrefu wa uwekezaji katika sekta hiyo, ambapo kuanzia upandaji hadi uvunaji wa miti huchukua takribani miaka 20, hali inayofanya taasisi nyingi za fedha kusita kutoa mikopo.
“Mfuko huu utawawezesha wazalishaji wadogo ambao wamekuwa wakipata changamoto kubwa ya mitaji.
Misitu na mnyororo wa thamani
Dk Makero amesema mfuko huo ni suluhisho muhimu kwa wahifadhi na wazalishaji wadogo, kwani utaimarisha uchumi wa wananchi huku ukiendeleza jitihada za utunzaji wa mazingira na misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Kuna wazalishaji wa mbegu, wapandaji wa miti kwa ajili ya magogo na mbao, wachakataji wadogo wa mazao ya misitu pamoja na wanaotumia mabaki kuzalisha bidhaa kama mkaa mbadala,” amesema Dk Makero.
Kwa upande wake, mwakilishi wa FAO nchini, Dk Tipo Nyabenyi amesema mradi huo unalenga kuweka mfumo endelevu wa kifedha utakaosaidia shughuli za urejeshaji wa misitu na ardhi zilizoharibika.
Amesema tofauti na miradi ya awali iliyotegemea ruzuku, mpango huu mpya unajikita katika utoaji wa mikopo kupitia taasisi za fedha kwa mashirika ya wakulima na wadau wa sekta binafsi, ambao watatakiwa kurejesha fedha hizo ili kuhakikisha mradi unaendelea kwa muda mrefu bila kutegemea misaada ya mara kwa mara.
“Lengo ni kujenga mfumo imara wa kifedha utakaohakikisha kuna mtiririko endelevu wa rasilimali kwa ajili ya kurejesha misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dk Tipo.