NINI kimeikuta Mtibwa Sugar? Ni swali unaloweza kujiuliza kufuatia timu hiyo kupoteza mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara chini ya Kocha Yusuf Chipo.

Chipo ambaye alitambulishwa Novemba 17, 2025 kuifundisha Mtibwa Sugar baada ya aliyeipandisha daraja timu hiyo, Awadh Juma kukosa vigezo vya kuwa kocha mkuu, alikuwa na mwendo mzuri mwanzoni katika mechi nane akitoka sare nne na ushindi mara nne, kabla ya kuanza kupokea vipigo hivyo mfululizo.

Kipigo cha leo Februari 25, 2026 cha mabao 3-0 kutoka kwa Azam ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, kimeishusha Mtibwa hadi nafasi ya saba.

Awali kabla ya mechi hiyo, Mtibwa ilikuwa nafasi ya tano na pointi zake 21 ikishuka dimbani mara 15.

Katika mechi ya leo, mapema dakika ya pili, krosi ya nahodha wa Azam, Lusajo Mwaikenda ikaunganishwa kwa kichwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ na kuukwamisha mpira nyavuni. Hilo ni bao lake la nne kwenye ligi msimu huu.

Bao hilo la mapema liliichanganya Mtibwa na kujikuta ikikosa utulivu hali iliyofanya dakika ya 19, krosi ya chinichini kutoka kwa Fei Toto, ikimaliziwa kiufundi na Jacques Ngita akiandika bao la pili na la kwanza kwake kwenye ligi.

Ngita akatupia bao la tatu dakika ya 59, baada ya kupokea pasi ya Mwaikenda, akamburuza beki wa Mtibwa, Eric Kyaruzi, kisha akachagua engo ambayo kipa Costantine Malimi akashindwa kudaka.

Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo, leo ilikuwa siku yake nzuri kutokana na kufungua akaunti ya mabao Ligi Kuu Bara, huku Fei Toto akifikisha mabao manne na asiti nne.

Azam imefikisha pointi 22 katika mechi kumi ilizocheza ikiendeleza rekodi ya kutopoteza katika ligi hiyo msimu huu sambamba na vinara Yanga. Azam katika mechi kumi, imeshinda sita na sare nne, imefunga mabao 16 na kuruhusu mawili. Imepanda kutoka nafasi ya nane hadi tano.

Mtibwa katika mechi 16 ilizocheza, imeshinda tano sawa na ilizopoteza, huku sare zikiwa sita. Imefunga mabao 13 na kuruhusu 17.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *