MANYARA: WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amemtaka kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara, Bahati Haule, kufanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha taarifa ya kila aliyehusika kuchukua fedha za mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto.

Dk Mwigulu amesema kuwa pamoja na kurejeshwa kwa fedha hizo, ni lazima hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya watumishi wote waliohusika na mpango huo ili kuimarisha uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma.

Amesema hayo leo Februari 26, 2026 baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto. Ofisi hiyo itagharimu kiasi cha Sh bilioni 1.85 hadi kukamilika kwake, na ujenzi wake umefikia asilimia 85.

“Kamanda wa TAKUKURU, ninataka uniletee taarifa hii kabla sijamaliza ziara yangu katika Mkoa wa Manyara. Ninahitaji taarifa za mtu mmoja mmoja kwa wote waliohusika kuchukua fedha hizo. Hatukutumwa kuja kuchukua fedha za umma, hatua za kinidhamu lazima zichukuliwe,” amesisitiza.

Kadhalika, Dk. Mwigulu amesema kuwa mbali na taarifa hiyo, anataka pia kuwasilishwa taarifa za mapato ya ndani, ikiwemo mapato yatokanayo na minada, zikionyesha namna yanavyokusanywa na kutumika. “Hakuna kuvumilia ubadhirifu wa mali ya umma. Tunataka kila mtu aheshimu fedha za utekelezaji wa miradi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dk. Mwigulu amesema kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati ya kutatua changamoto za Watanzania, akisisitiza kuwa lengo lake ni kuona maendeleo endelevu yanapatikana nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *