SAA chache tangu awaage wachezaji aliofanya nao kazi Transit Camp, Kocha Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ amekiri ana kazi kibarua kikubwa cha kufanya kuhakikisha timu anayokabidhiwa inarudi kwenye ushindani.

Nsajigwa, amekabidhiwa kuinoa Tanzania Prisons akichukua mikoba ya Zedekiah Otieno ambaye tayari wamefikia makubalianao ya pande mbili kusitisha mkataba wake akiwa ameiongoza timu hiyo kwenye mechi 14.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nsajigwa alisema anatambua majukumu anayoenda kukabiliana nayo Prisons kutokana na timu kutokuwa katika nafasi nzuri ya ushindani, lakini anaamini kila kitu kitaenda vizuri mara baada ya kukaa na wachezaji sambamba na viongozi.

“Mimi ni kocha sitakiwi kukimbia kazi kwa kuhofia matokeo mabaya yaliyopita. Kila kocha ana mbinu zake. Naenda kufanyia kazi nilichonacho kwa kuipambania timu iweze kutoka kwenye nafasi mbaya iliyopo na kuwa timu shindani. Natarajia ushirikiano wa kutosha.

“Naenda kuongoza kundi la wachezaji wazoefu na bora. Naamini watafanya kazi nzuri pamoja na mimi ili tuweze kuitoa timu katika nafasi iliyopo na kuipelela mbele zaidi ikiwa timu shindani.”

Wakati huo huo, alitumia nafasi hiyo kuwatakia kila la kheri waajiri wake wa zamani katika kuhakikisha wanaipambania timu kuendelea kuwa bora na hatimaye kufikia malengo.

“Nimewaaga sio tu kama wafanyakazi wenzangu, bali kama familia yangu ya pili. Kipindi tulichokuwa pamoja, kilikuwa zaidi ya mpira, kilikuwa ni safari ya upendo, mshikamano, kujifunza na kukua pamoja.

Nimejifunza mengi kupitia viongozi wetu, wachezaji wangu na mashabiki waliotuunga mkono kila hatua katika Kutafuta ushindi uwanjani, ushirikiano wenu umeacha alama kubwa moyoni mwangu.

“Naanza safari mpya katika timu ya daraja la juu, lakini moyo wangu utaendelea kubeba kumbukumbu na heshima kubwa kwenu. Nawashukuru sana kwa sapoti, ushirikiano na urafiki wa kweli. Nawatakia mafanikio makubwa zaidi, malengo yenu yatimie, tuendelee kuwa na furaha, umoja na mshikamano ndani na nje ya uwanja.”

Hiyo ni sehemu ya maneno ya Nsajigwa akiwaaga Transit Camp.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *