
Shirika moja la haki za kisheria limebaini kile lilichokitaja kuwa “juhudi za kimfumo” za kukandamiza harakati za mshikamano na Palestina nchini Uingereza, likirekodi karibu matukio 1,000 katika kipindi cha miaka sita iliyopita yanayoonesha mfumo uliokita wa “ukandamizaji dhidi ya Wapalestina.”
Kituo cha Ulaya cha Msaada wa Kisheria (European Legal Support Center – ELSC) kimesema kilithibitisha kesi 964 kati ya mwaka 2019 na Agosti 2025, zinazohusisha kukamatwa kwa watu, adhabu kazini, kufutiwa viza, uchunguzi wa vyuo vikuu, na kufutwa kwa matukio—yote yakihusishwa na misimamo au matamshi ya kuunga mkono Palestina.
Kwa kushirikiana na watafiti kutoka Forensic Architecture, shirika hilo lilichapisha kesi hizo katika “Index of Repression”, hifadhidata ya wazi inayolenga kuchora ramani ya mienendo ya ukandamizaji katika taasisi mbalimbali, zikiwemo vyuo vikuu, waajiri, kumbi za kitamaduni na vyombo vya serikali.
Kwa mujibu wa ELSC, matukio hayo yanaakisi shinikizo lililoratibiwa linalolenga kuwasilisha uungaji mkono wa Palestina kama suala la kiusalama badala ya msimamo halali wa kisiasa. Shirika hilo linasema athari zake zimeenea kutoka vyuoni hadi sehemu za kazi, na kuleta mazingira ya hofu na kujizuia kujieleza hadharani.
Miongoni mwa kesi zilizobainishwa ni ya mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Warwick aliyekamatwa baada ya kuonesha bango la maandamano wakati wa mkutano wa chuo mwishoni mwa mwaka 2023.
Hifadhidata hiyo pia inarejelea kufutiwa viza kwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Manchester baada ya kutoa maoni kwa Sky News kuhusu vita vya mauaji ya kimbari vya Israel huko Gaza. Uamuzi huo ulifutwa baada ya rufaa mwaka 2024.
Ripoti ya ELSC pia inaeleza kuhusika kwa makundi ya watetezi wa Israel, yakiwemo UK Lawyers for Israel, katika kuwasilisha malalamiko katika kesi nyingi.
Matokeo haya yanatolewa wakati ambapo maandamano ya kuunga mkono Palestina yanaendelea kuvuta umati mkubwa kote Uingereza, sambamba na kile kinachoelezwa na mashirika ya haki za binadamu kuwa ni kampeni inayoendelea ya mauaji ya kimbari na utakaso wa kikabila huko Gaza, iliyoanza Oktoba 2023.