DAR ES SALAAM: MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amebainisha mafanikio ya Kampuni ya Ndege ya ATCL, ambapo amesema kuwa hadi sasa imefanikiwa kuingiza zaidi ya dola za Marekani milioni 157.

Akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa Julius Nyerere International Airport jijini Dar es Salaam, Msigwa amesema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la idadi ya abiria.

Amefafanua kuwa idadi ya abiria imeongezeka kutoka 822,232 katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi zaidi ya abiria 1,400,000 katika kipindi cha 2025/2026, hatua inayoonesha ukuaji mkubwa wa kampuni hiyo katika soko la usafiri wa anga.

Katika kuendeleza mafanikio hayo, Msigwa amesema serikali imepanga kununua ndege mpya nane, hatua itakayoongeza idadi ya ndege kutoka 16 za sasa hadi kufikia 24, zikihudumia safari za ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa upanuzi huo unaenda sambamba na mkakati wa serikali wa kuboresha na kupanua viwanja vya ndege nchini ili kuongeza wigo wa huduma, kuimarisha ushindani, na kuvutia abiria zaidi.

Kwa mujibu wa Msigwa, hatua hizo pia zinalenga kuimarisha sekta ya utalii pamoja na kuongeza ufanisi wa ATCL katika soko la kimataifa la usafiri wa anga.

Serikali ina matumaini kuwa kwa kuongeza idadi ya ndege na kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege, ATCL itaendelea kuimarika kibiashara na kuchangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya usafiri wa anga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *