SIMIYU: Serikali imeitaka Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala kuendelea kutatua changamoto zote zilizopo katika mfumo stakabadhi ghalani kwani ndiyo mfumo ambao umeonyesha mafanikio makubwa katika kumlinda Mkulima.
Aidha, bodi hiyo imetakiwa kuweka nguvu zaidi katika kuwawezesha wadau wote ili wawezesha kushiriki kikamilifu katika mfumo huo kuanzia shambani hadi sokoni na siyo kubaki katika kazi ya kudhibiti pekee yake.
Maagizo hayo yametolewa jana mjini Bariadi mkoani Simiyu na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga wakati akifunga msimu wa matumizi ya mfumo wa stakabadhi za ghala 2025/2026 na kufungua msimu mpya wa matumizi wa mfumo huo 2026/2027.
Alitaka bodi hiyo kuendelea kutoa elimu ya uelewa kwa wadau wote ili waweze kushiriki kikamilifu katika mfumo huo bila ya kuwepo malalamiko, huku akiagiza kuhakikisha changamoto zote ambazo zimekuwa zinajitokeza ziweze kutatuliwa haraka.
“Nimeambiwa hapa kuwa kuna changamoto ya maghala yasiyokidhi vigezo na mmeniambia nitoe tamko la kupiga marufuku hayo maghala, hiyo hapana mnatakiwa kuwawezesha wenye maghala ili yaweze kuwa bora na siyo kuwafungia,” alisema Waziri Kapinga.
Waziri Kapinga alisema kuwa katika msimu ambao umeisha wa 2025/2026 mfumo huo umeonyesha mafanikio makubwa kwa mazao ya wakulima ambayo yaliuzwa kupitia minada ya stakabadhi ghalani.
Alisema kuwa katika msimu huo jumla ya tani milioni 1.13 zilikusanywa kupitia mfumo huo, ambapo kiasi cha Sh trioni 2.4 zililipwa kwa wakulima, bilioni 65 zililipwa kwa halmashauri kama ushuru huku zikipatikana ajira rasmi 1,430 na zisizokuwa rasmi zaidi ya 1,000.
Alisema kuwa jumla ya mazao nane yaliuzwa kupitia mfumo huo, ambayo ni Choroko, Korosho, mbaazi, dengu, kahawa, soya, kakao, na ufuta, ambapo kupita mfumo huu wakulima wamenufaika na kupata bei halisi ya soko.
“Serikali tunaamini mfumo huu una manufaa makubwa kwa wadau wote, wakulima, wafanyabiashara na serikali, msimamo wa serikali lazima mfumo huu utumike na uwepo, ni jambo ambalo halina mjadala na ndiyo maagizo ya Rais Dk Samia,” alisema Kapinga.
Alisema kuwa serikali itaendelea kufanya maboresho makubwa katika mfumo huo ili kuhakikisha mazao yote ya shambani ya wakulima yanauzwa kupitia mfumo huo na wakulima wanaendelea kunufaika.
