Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua magari maalumu ya kutolea huduma za kodi maarufu ‘ofisi zinazotembea’ ili kuboresha huduma na kuzisogeza karibu na wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa magari hayo jana Jumatano, Februari 25, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar alisema yatasaidia kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za kodi na kurahisisha ulipaji wa kodi nchini.

Amesema magari hayo yatakayotumika kama ‘ofisi zinazohama’ yamezinduliwa sambamba na magari mengine 72 ya kutolea huduma za kodi ambayo yatakuwa chachu ya ulipaji kodi kwa hiari, kwani huduma zitawafuata wananchi walipo.

“Nawapongeza TRA kwa ubunifu huu wa kuwafuata wananchi ili kuwahudumia katika maeneo yao, hali hii itaongeza kasi ya ulipaji kodi sambamba na makusanyo ya mapato kuelekea kuiwezesha Tanzania kujitegemea kwa kiasi kikubwa kiuchumi,” amesema Balozi Khamis.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Uledi Abasi amesema huo ni miongoni mwa mikakati ya mamlaka hiyo ya kujiweka karibu zaidi na wananchi na kuboresha huduma za kodi.

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema uzinduzi wa ofisi zinazohama na magari ya kutolea huduma za kodi ni miongoni mwa mikakati ya kuimarisha huduma kwa walipakodi.

Amesema kupitia magari hayo wataweza kuwafuata walipakodi na kuwapatia huduma zote za kodi katika maeneo yao.

Mwenda amesema magari haya ni ofisi zilizokamilika ambazo zitatoa huduma zote zinazopatikana kwenye ofisi nyingine za TRA hivyo ametoa wito kwa wananchi kuyatumia ipasavyo.

Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliohudhuria uzinduzi huo wamesema yatarahisisha utoaji wa huduma kwenye maeneo yao badala ya kulazimika kuzifuata kwenye ofisi za TRA.

Omar Hemed, mfanyabiashara wa Tegeta amesema:”Tunashukuru mmezindua ofisi hizi ambazo tunaamini sisi wafanyabiashara wa sokoni Tegeta Nyuki zitatufikia na kutuwezesha kupata huduma za kodi ikiwemo TIN.”

“Tunaomba huduma hizi zitufikie sisi waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda njiapanda ya Mabwepande, ili tupate TIN kwa urahisi sambamba na leseni za udereva,” amesema mwenyekiti wa waendesha bodaboda Mabwepande.

Mkazi wa Tabata, Mariam Juma ameiomba TRA kuboresha huduma zake zaidi kama hivyo kwa kuwafuata wananchi walipo lakini kuendelea kutoa elimu ya ulipa koji kwa hiari.

“Wananchi wakipata elimu nzuri ya ulipaji kodi watalipa, ule utamaduni wa mabavu si mzuri na sasa siuoni, waendelee hivyo kama ambavyo Rais alisema hataki kodi za mabavu,” amesema Mariam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *