Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa tuzo za ubunifu kwa washindi tisa waliowasilisha mawazo bora yaliyolenga kuboresha huduma za kodi na kuongeza wigo wa walipakodi nchini.

Akikabidhi tuzo hizo leo Jumanne Februari 25, 2026, Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar, ameipongeza TRA kwa kuanzisha tuzo hizo akisema zitasaidia kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Amesema jukumu la kulipa kodi ni la kila mwananchi, hivyo hata washiriki ambao hawakushinda wametoa mchango muhimu katika jitihada za kupanua wigo wa kodi kwa kuonesha uelewa wa umuhimu wa zoezi hilo.

New Content Item (4)

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Uledi Abasi, amesema utoaji wa tuzo hizo unalenga kuifanya TRA kuwa karibu zaidi na wananchi sambamba na kuongeza wigo wa kodi.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda, amesema mpango wa tuzo za ubunifu ni endelevu na kwamba kwa mwaka wa fedha 2025/2026 dirisha la kupokea mawazo litafunguliwa Aprili 1 hadi Juni 30, 2026, huku muongozo wa namna ya kuandaa na kuwasilisha mawazo ukitarajiwa kutolewa kabla ya kipindi hicho.

Mwenda amesema mawazo bunifu yatasaidia TRA kuboresha huduma zake, kuongeza walipakodi na hatimaye kuongeza makusanyo ya Serikali, jambo litakalowezesha kupunguza viwango vya kodi kwa muda mrefu.

New Content Item (4)

“Ni matarajio ya walipakodi kuwa wigo ukiongezeka viwango vya kodi vitapungua. Sisi pia tunayo matarajio hayo ndiyo maana tunafanya juhudi za kuongeza wigo wa kodi,” amesema Mwenda.

Katika tuzo hizo, mshindi wa jumla Gabriel Mashenene amejinyakulia Sh50 milioni, huku washindi watatu wakipata Sh30 milioni kila mmoja na washindi watano wakizawadiwa Sh20 milioni kila mmoja.

Jumla ya mawazo bunifu 5,681 yaliwasilishwa katika shindano hilo; kati yake mawazo 106 yalichaguliwa kwa hatua ya awali kabla ya kubaki mawazo tisa yaliyoshinda na kupewa tuzo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *