Iringa. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewaagiza wahandisi, makandarasi na kampuni zinazotekeleza miradi ya Serikali, kuhakikisha kila fundi au kibarua anayeshiriki katika miradi hiyo anapewa cheti maalumu baada ya kukamilika kwa mradi, kinachoonesha amefanya kazi husika.

Agizo hilo amelitoa leo Alhamisi Februari 26, 2026, wakati wa ziara yake katika mradi wa ujenzi wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Nduli, Manispaa ya Iringa, unaogharimu Sh41.66 bilioni.

Waziri Ulega amesema lengo la utaratibu huo ni kuwasaidia vijana wengi wanaofanya kazi katika miradi ya ujenzi kujijengea sifa na uzoefu utakaowawezesha kupata ajira nyingine pindi miradi inapokamilika.

Waziri wa ujenzi nchini, Abdallah Ulega, akitoa agizo la kila kibarua kupewa cheti atakapomaliza kufanya kazi katika mradi wa ujenzi wa serikali, Leo Februari 26, 2026 wakati wa ziara yake katika mradi wa ujenzi wa jengo la abiria Uwanja wa Ndege Nduli Manispaa ya Iringa. Picha na Christina Thobias

“Vijana wanaoshiriki katika kazi hizi lazima wapewe vyeti vinavyoonesha walifanya kazi hiyo. Inaweza kutokea nafasi nyingine ya kazi na kijana ameishia darasa la saba; cheti hicho kitamjenga na kumsaidia kuomba kazi nyingine,” amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia ukiukwaji wa haki za wafanyakazi, akieleza kuwa fedha zinazotumika katika miradi hiyo ni za Watanzania na zinapaswa kusimamiwa kwa uadilifu.

“Hii ni pesa ya Watanzania, ni pesa yetu sisi. Makandarasi wanafanya kazi kwa kushirikiana na vibarua, hivyo ni wajibu wao kuwalipa kwa wakati. Ni marufuku kuchezea fedha za wafanyakazi,” amesisitiza.

Vilevile, Waziri Ulega ameonya kuwa hakuna mfanyakazi anayepaswa kufukuzwa kazi kwa kudai haki yake. Amewataka viongozi wa wilaya na mkoa kusimamia kwa karibu masuala ya masilahi ya wafanyakazi ili kuhakikisha haki inatendeka.

“Hakuna kuwafukuza vijana kwa sababu ya kudai malipo yao. Viongozi wa wilaya na mkoa hakikisheni wanaodai haki zao hawafukuzwi kazi. Afukuzwe mdokozi, mwizi au mdanganyifu, lakini si mtu kwa sababu ya kudai haki yake,” amesema.

Kuhusu nidhamu kazini, Waziri Ulega amewataka wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuepuka mazoea yasiyo na tija.

“Hapa ni kazi, na tunataka mfanye kazi hadi mwisho wa mradi. Hakikisheni mnafanya kazi kwa nidhamu na kwa weledi, si kwa mazoea au kupoteza muda. Haya ni maisha yenu,” amesema.

Waziri wa ujenzi nchini, Abdallah Ulega Leo Februari 26, 2026 akizungumza na Uongozi wa mkandarasi anayetekeleza mradi wa jengo la abiria, China Harbour Engineering Company Ltd (CHEC) uwanja wa ndege Nduli uliopo Manispaa ya Iringa na kuwasihi kuhakikisha haki zinazingatiwa kazini. Picha na Christina Thobias

Pia amekemea vitendo vya unyanyasaji kazini, akionya kuwa makandarasi hawaruhusiwi kuwapiga au kuwanyanyasa wafanyakazi wao.

“Makandarasi hawaruhusiwi kupiga mtu, na ikitokea tena hatua kali zitachukuliwa,” ameonya.

Akitoa taarifa ya utekelezaji Meneja wa mradi huo, Rehema Shabenga amesema umefikia hatua nzuri ya utekelezaji.

Amekiri kulikuwepo na changamoto ya ucheleweshaji wa malipo kwa baadhi ya vibarua, jambo lililoathiri utendaji kazi.

“Suala la kucheleweshewa malipo si zuri, kwa sababu lilisababisha kazi kusimama kwa siku tatu,” amesema Shabenga.

Akizungumzia umuhimu wa mradi huo, Waziri Ulega amesema kwa sasa jengo la abiria lililopo lina uwezo wa kuhudumia abiria 14 na magari 30 kwa wakati mmoja, lakini jengo jipya linalojengwa litaongeza uwezo huo hadi kufikia abiria 120 kwa wakati mmoja.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Iringa, Yudas Msangi amesema mradi huo una mchango mkubwa katika kuboresha miundombinu ya usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.

Meneja wa mradi wa jengo la abiria uwanja wa ndege Nduli, Rehema Shabenga, (Anayetoa maelekezo kwenye mchoro)akitoa taarifa ya mradi jinsi unavyokwenda mpaka sasa.Picha na Christina Thobias

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta amesema uwanja huo ni muhimu katika kurahisisha usafiri na kukuza sekta ya utalii mkoani humo.

Amesema ujenzi wa jengo jipya lenye uwezo mkubwa wa kuhudumia abiria utaongeza fursa za kiuchumi na kijamii.

Mmoja wa wafanyakazi wa mradi huo, Salum Kisoma, amesema kwa sasa hali ni nzuri tofauti na awali kulipokuwapo sintofahamu kuhusu mishahara.

“Kwa sasa mambo yanaenda vizuri, lakini kulikuwa na changamoto ya ucheleweshaji wa mishahara. Pia kulikuwa na tukio la raia wa kigeni kumpiga mfanyakazi, jambo lililotuumiza sana,” amesema Kisoma.

Kabla ya ziara kumalizika, wafanyakazi hao waliomba kupewa namba ya simu ya waziri ili waweze kuwasiliana naye moja kwa moja endapo changamoto zitajitokeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *