Musoma. Kesi inayowakabili watuhumiwa wanne wanaodaiwa kushiriki katika wizi wa gari la kubeba wagonjwa mali ya Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara imeahirishwa hadi machi 12,2026 kutokna na upelelezi kutokamilika.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi yenye namba 3139/2026 ilikuja leo Februari 26,2026 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Musoma ikiwa ni mara ya pili ambapo awali ilifikishwa mahakamani hapo Februari 13,2026
Washtakiwa hao wanadaiwa kuiba gari hilo na kulipeleka mkoani Arusha kisha kulibadilisha na kuwa gari la biashara ya kubeba watalii.
“Upelelezi bado haujakamilka hivyo mtarudi tena mahakamani hapa Machi 12,2026 kwa ajili ya kesi yenu kutajwa,” amewaambia washtakiwa .
Washatakiwa wa wizi wa gari la kubeba wagonjwa mali ya Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, wakitoka mahakamani baada ya kesi yao kuahirishwa hadi Machi 12, 2026. Picha na Beldina Nyakeke
Awali, wakili wa Serikali, Agma Haule amesema upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea hivyo kumuomba hakimu kupanga tarehe nyingine ya kesi hiyo kutajwa mahakamani hapo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Goodluck Chacha (26) ambaye ni dereva na mkazi wa Tarime mkoani Mara na Karume Kihedu (26) fundi makenika na mkazi wa Arusha.
Wengine ni Saidi Ramadhani (39) fundi makenanika pamoja na Elias Joakim (53) wote wakazi wa Arusha.
Washtakiwa wote wanne wanashtakiwa kwa kosa la utakatishaji wa fedha kinyume cha Kifungu 12(d) na 13(a) ya sheria ya udhibiti utakatishaji wa fedha sura namba 423 ambayo inasomwa pamoja na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha sheria ya uhujumu uchumi na udhibiti wa uhalifu wa kupanga.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kupokea kiasi cha Sh55 milioni kutoka kwa Alexia Baraka huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu na kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Washatakiwa wa wizi wa gari la kubeba wagonjwa mali ya Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, wakitoka mahakamani baada ya kesi yao kuahirishwa hadi Machi 12, 2026. Picha na Beldina Nyakeke
Katika kesi hiyo, mshatkiwa wa kwanza pia anashtakiwa kwa kosa la wizi kinyume na kifungu cha 258 (1) na 265 (1) ya sheria ya kanuni ya adhabu sura namba 16 marejeo ya 2023.
Anadaiwa kufanya kosa hilo katika Manispaa ya Musoma eneo la maegesho ya magari lililopo ndani ya manispaa ambapo inadaiwa kuwa aliiba gari aina ya Toyota Landcruiser mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lenye thamani ya Sh180 milioni.
Pia mshatiwa huyo wa kwanza anashtakiwa kwa tuhuma za kuongoza genge la uhalifu kinyume na aya ya 4(1) (d) ya jedwali la 1 kifungu cha 57(1) na 60 (2) cha sheria ya uhujumu uchumi na udhibiti wa uhalifu wa kupangwa sura namba 200 marejeo ya mwaka 2023.
Chacha anadaiwa kufanya kosa hilo Oktoba 25, 2025 na Oktoba 27,2025 katika maeneo tofauti ndani ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara na Arusha ambapo anadaiwa kuhamasisha biashara ya uhalifu kwa nia ya kupata faida kinyume cha sheria.